Monday, October 3, 2016

FAIDA NA CHANGAMOTO ZA KAZI YA BODABODA - KAGERA

Na Frank Johnson
Biashara ya bodaboada ni biashara inayokuwa kwa kasi sana mkoani Kagera,ikianzia nchi ya jirani Uganda na kwa Tanzania naweza sema Kagera ndio Mkoa wa kwanza kufanya biashara hii ya bodaboda.Vijana wengi kutokana na ukosefu wa ajira wameamua kuingia kwenye biashara ya bodaboda.Kwa mkoa wa Kagera biashara ya bodaboda imekuwa ni fursa kwa vijana kutokana na ukosefu wa usafiri wa magari kutoka sehemu moja kwenda nyingine mfano mtu anayetoka Kahororo,Kashai au Mafumbo akitaka kwenda mjini ni lazima achukue bodaboda au atembee kwa mguu.
Gazeti la Hamasa limefanikiwa kuzungumza na waendesha bodaboda pia wamiliki wa bodaboda kujua ni changamoto gani na faida wanazopata kutoka kwenye bodaboda,tulizungumza na waendesha bodaboda kutoka wilaya ya Bukoba,Karagwe,Misenyi,Muleba,Biharamulo,Ngara na Kyerwa.
Kutokana na malezo yao,kwenye kufanya hii biashara ya bodaboda kuna njia mbili,moja ni kumwachia  ni kuwa na mkataba, wamiliki uwapa waendesha bodaboda na uhitaji kupewa kiwango cha pesa kuanzia Tsh 7,000 hadi Tsh 10,000 na baada yamwaka mmoja inakuwa ya muendesha bodaboda baada ya mkataba kuisha,aina ya pili ni bila mkataba mmiliki hupewa kuanzia Tsh 6,000 hadi Tsh 8,000 kwa siku kulingana na eneo husika.
Mkoani Kagera changamoto na faida wanazopata bodaboda tulizobaini kutokana na kufanya nao mahojiano kutoka katika wilaya zote ni,wizi na uporaji umeongezeka,kama ilivyo changamoto kwenye biashara nyingine,waendesha bodaboda wengi wameibiwa na kuporwa pikipiki na watu wanaojifanya kuwa abiria lakini baadaye wanawageuka na kuwapora kwa kuwatishia kuwafanyia jambo baya.
Changamoto nyingine ni ajali kuongezeka,hii inasababishwa na vijana wengi kutokujua sheria za barabara,kuna vijana wanaamini ukishajua kuendesha bodaboda mtaani unaweza pia kuendesha barabarani,hii hupelekea waendeshe pikipiki barabarani bila kuwa na uelewa kuhusu sheria za barabara.Ajali nyingi zimepelekea vifo na ulemavu wa kudumu kuongezeka. Changamoto nyingine waliyotuambia ni kupata vishawishi vya ngono, kuna abiria ambao ni wanawake wakipandapikipiki hawataki kulipa na kuwambia kuwa wanaweza kulipa kwa kufanya ngono hasa abiria ambao wanawachukua usiku kutoka sehemu za starehe.Hii inapelekea magonjwa ya zinaa kuongezeka,mimba zisizotarajiwa na watoto wanaozaliwa kukosa malezi pia ni hasara kwa muendesha bodaboda na mmiliki kwa kukosa mapato sahihi.
Changamoto nyingine tuliyoigundua Hamasa ni kuwa watoto wanaugua ugonjwa wa nimonia kwa kuwekwa mbele kabisa kwenye pikipiki,kutokana na upepo mkali hii inapelekea watoto kupata ugonjwa wa nimonia.
Pia waendesha bodaboda na wamiliki wake mkoani Kagera wametueleza faida wanazopata kutokana na biashara hiyo ya bodaboda. Moja imekuwa mkombozi wa tatizo la ajira,biashara ya bodaboda imeleta ajira kwa vijana,vijana wengi mkoani Kagera wamejiajiri kwenye bodaboda na kuajiriwa pia kutokana na biashara hii,hivyo inawaongezea kipato.Pia imeleta ajira kwa mafundi ambao hutengeneza hizo bodaboda pale zinapoharibika au kuzifanyia matengenezo.
Pili vipato vya ziada vya wafanyakazi binafsi na wale wa serikali kama waalimu vimeongezeka,wafanyakazi wengi wamechukua mikopo na kununua bodaboda ili kuwapa vijana waendeshe kwa ajili ya kuwaongezea kipato cha ziada,wafanyakazi wengi wananufaika kutokana na hii biashara ya bodaboda mkoani Kagera.
Tatu imerahisisha usafiri maeneo ya mjini na vijijini pia,kuna maeneo mengi mkoani Kagera kabla ya biashara ya bodaboda kuingia wananchi walikuwa wanapata shida ya usafiri na kuwalazimu kutembea umbali mrefu kwa mguu,lakini sasa kutokana na uwepo wa bodaboda imerahisha usafiri mjini na vijijini. Mwisho serikali imeingiza mapato na inazidi kuingiza

mapato kutokana na biashara hii ya bodaboda, kuanzia pikipiki zinapoingia Tanzania hadi biashara inapofanyika.
Hasara ya hii biashara ni kwamba imesababisha vilema vingi sana, watu wengi wamepata vilema kutokana na matumizi mabovu ya usafiri huu.
Gazeti la Hamasa linatoa wito kwa serikali ya mkoa wa Kagera kuwa wanatoa elimu mara kwa mara kwa waendesha bodaboda kuhusu usalama barabarani pia wamiliki wa bodaboda kuhakikisha mtu wanayempa chombo cha usafiri ana leseni.Vilevile tunatoa wito kwa waendesha bodaboda kuzingatia sheria za barabarani na kutotumia kilevi chochote muda wa kazi.

Madereva bodaboda wakiwa wamepack jirani na soko kuu la manispaa ya Bukoba

No comments:

Post a Comment