Monday, October 3, 2016

FIESTA MULEBA


Lile tamasha kubwa la Muziki Tanzania, FIESTA linaloandaliwa na Clouds Entertainment siku ya tar 28 Agosti lilitua mjini Muleba kwenye kiwanja cha Zimbihile ambapo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kukata kiu ya mashabiki wa muziki wa kizazi kipya ‘BongoFleva’ wa maeneo hayo na maeneo ya jirani kwa kushuhudia wasanii wengi wakubwa wakitumbuiza laivu, lakini pia kupitia jukwaa la Fiesta tuliweza kuvitambua vipaji vipya vya nyumbani, kwani kulikuwa na msululu wa zaidi ya wasanii 30 waliopewa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao kutoka mkoani Kagera.

Orodha ya wasanii wa Dar es salaam waliotumbuiza ni; Shilole, Mr Blue, Maua Sama, Bilnas, Jux, Raymond, Nandy, Baraka Da Prince, Darasa, Stamina, Navy Kenzo, Chege, Christian Bella, Msami, ManFongo, Shollo Mwamba, Edo Boy na Bonge La Nyau.

Wasanii waliofanikiwa kupata shangwe nyingi ni Joh Makini, Stamina, Mr. Blue, Chege, Baraka De Prince na Jux huku katika hali isiyotarajiwa yule mkali wa kisingeli Man Fongo ‘Nshomile’ wakashindwa kumuelewa kabisa na kubaki wakimuangalia tu mda mwingi alipokuwa jukwaani bila kumpa ushirikiano wowote.

Pia kwa upande wa wasanii wa nyumbani ni wengi sana waliopata nafasi ya kupanda jukwaani, wasanii zaidi ya 30 walipata nafasi hiyo huku msanii aliyetambulika kwa jina la Love B akionekana kufunika zaidi na michano yake (Rap) sambamba na msanii Obed Moses ‘O-Strings’ aliyefanikiwa kuibuka mshindi wa shindano la super nyota, na kupata nafasi ya kwenda Dar es salaam kwa ajili ya fainali za shindano hilo. Msanii mwingine wa nyumbani aliyeonekana kukubalika ni Mr. Mos aliyepigiwa shangwe baada ya kuimba wimbo wake wa ‘Kazi ya kidole’.

Gazeti la HAMASA lilijaribu kupiga stori na wadau wawili waliohudhuria Tamasha la FIESTA la mwakajuzi Kaitaba mjini Bukoba na hili la Muleba kiwanja cha Zimbihile na kusema hili la mwaka huu ni ‘funiko’, watu walikuwa wengi zaidi na wasanii waliotumbiza walijipanga sana.
Hili limekuwa kinyume na matarajio ya wengi, wakidhani Tamasha lingekosa mvuto kutokana na kushindwa kufanyika Bukoba mjini .













No comments:

Post a Comment