Monday, October 3, 2016

UWANJA WA KAITABA NI KWA AJILI YA LIGI KUU TU

BUKOBA MICHEZO                          

Siku chache baada ya uwanja wa kaitaba kukamilika,wananchi mkoani Kagera wameshauriwa kuacha mazoea ya kutumia uwanja huo kama ilivyokuwa zamani ikiwa ni pamoja na kuwekwa utaratibu na ratibainayoeleweka kwa matumizi ya uwanja huo. Akiongea na gazeti hili afisa michezo wa mkoa  kagera bw. Kepha Elius alisema kuwa kwa ushauri waliopewa na kandarasi wa uwanja huo,alisema ni vyema utumike kwa michezomichache ili uweze kupata muda wa kupumzishwa kwani unaweza kudumu kuanzia miaka 8-15 bila kuharibika,huku akishauri kuwa ni bora uwanja huo utumike kwa michezo ya ligi kuu na kwa ligi za kawaida uwepo utaratibu wa kutumia viwanja vingine lakini hata ikiwa kaitaba isiwe kila mara.

Kwa upande mwingine Bw.Kepha alilipongeza shirika la Jambo Bukoba kwa mpango wao mzuri wanaoendelea nao wa kuboresha uwanja wa Nshamba Tapa uliopo wilayani Muleba na uwanja wa Kihanga uliopo wilayani Karagwe,maana hali hiyo itaupunguzia mzigo uwanja wa Kaitaba ikiwa ni pamoja na kuendelea kukuza vipaji vya michezo mkoani Kagera.
Kufuatia hali hiyo amezishauri halmashauri zote mkoani Kagera kuendelea kuboresha viwanja vya michezo katika maeneo yao na kusimamia michezo ya aina zote,na kuongeza kuwa halmashauri ya manispaa ya Bukoba inatakiwa kukamilisha maboresho ya maeneo mengine  katika uwanja wa kaitaba na aliwapongeza kwa hatua nzuri waliofikia tangu walipokabidhiwa uwanja huo na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania(TFF).
Akiongelea muamko wa michezo mkoani Kagera alisema kuwa bado wanakabiliwa na changamoto ya wadhamini,na wakipatikana wanajikita zaidi kwa mchezo mmoja wa mpira wa miguu hali inayoendelea kudidimiza  michezo mingine mkoani  humo,na aliwaomba wafadhili kubadilika na kuwa na muamko kwa michezo yote ili  kuwasaidia wanakagera wenye vipaji katika Michezo hiyo.
Katika hatua nyingine bw.Kepha alisema kuwa  mkoa wa Kagera upo kwenye mpango wa kuanzisha mchezo wa mbio za polepole(Jogging club)ambao utasaidia kuimarisha afya kwa watakaopenda kushiriki,na aliongeza kuwa kupitia hapo wataweza kufanya hata mazoezi mbalimbali ya viungo vya mwili ambayo yatakuwa yanafanyika katika wiki ya usafi ya mwisho wa mwezi  kuanzia saa kumi na mbili za asubuhi  kwa kuzunguka maeneo mbalimbali katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Uwanja wa Kaitaba uliopo Manispaa ya Bukoba kama unavyoonekana kwa sasa

No comments:

Post a Comment