Monday, October 3, 2016

MFAHAMU MWANZILISHI WA FACEBOOK (SEHEMU YA KWANZA}

NA DIDAS MUGYABUSO
(Kwa msaada wa tovuti mbalimbali)



Mark Elliot Zuckerberg alizaliwa Mei 14, 1984, eneo la White Plains, New York, ni mtoto wa pekee wa kiume na wa pili kuzaliwa kwa mama Karen Zuckerberg, daktari wa  magonjwa ya akili na baba Edward Zuckerberg, daktari wa meno. Yeye na dada zake watatu; Randi, Donna, na Arielle, walikulia Dobbs Ferry, New York. Uwezo wake wa kuandika programu haukuibuka kama miujiza, alianza kuvutiwa na masomo ya kompyuta tangu utotoni, akiwa na miaka 10 alipata kompyuta yake ya kwanza aina ya Quantex 486DX  kipindi hicho ni mwanafunzi wa shule ya kati, akiwa na miaka 12 babayake alimfundisha Lugha ya kikompyuta inayoitwa Atari Basic Programming
miaka ya 1990, aliitumia lugha hiyo kutengeneza mesenja ambayo aliiita ZuckerNet, iliziunganisha kompyuta zote zilizopo nyumbani kwao na ofisi ya babayake ya magonjwa ya meno iliyokuwa jirani na nyumba yao. Babayake aliiweka mesenja kwenye kompyuta yake ya ofisini na mtu wa mapokezi aliweza kumtaarifu  mgonjwa mpya anapoingia ofisini kwa kutumia programu hiyo. Babayake Edward Zuckerberg alikuwa akim’sapoti’ sana mtoto wake, baada ya kugundua ana kitu ndani yake, ilifika kipindi akamkodi mwalimu wa kompyuta ‘software developer’ David Newman ili amfundishe mtoto wake kama mwalimu binafsi. Newman alimwita mwanafunzi wake ‘mwenye akili nyingi’, kiasi kwamba ilikuwa vigumu kumtangulia. Zuckerberg pia alichukua mafunzo ya somo hilo katika Chuo cha Mercy, jirani na nyumbani kwao, alipokuwa bado akisoma ‘high school’. Alifurahia kujifunza programu za kompyuta, hasa vifaa vya mawasiliano na michezo. Pia alipokuwa elimu ya juu ‘High School’ aliandika code na kufanikiwa kutengeneza programu ya kucheza mziki aliyoiita Synapse Media Player kwa ajili ya kucheza miziki iliyo kwenye mfumo wa MP3,programu hiyo ilikuwa na uwezo wa kujua mtumiaji anapendelea miziki ya namna gani na kuweza kumtengenezea mtumiaji ‘playlist’ ya miziki kwa kukisia miziki anayopenda mtumiaji. Makampuni makubwa  ya Teknolojia duniani kama Microsoft na AOL walivutiwa sana na ujio wa programu hiyo ya Synapse Media Player na kila moja ilikuwa ikimshawishi Mark kuwauzia programu hiyo kwa kumtumia ofa nzuri, hata hivyo ‘jiniazi’ huyo alikataa ofa hizo za makampuni hayo mazito duniani, na alikataa ofa ya kushirikiana nao katika kazi. Aliendelea kukataa ofa hizo zilizokuja mara kwa mara za kuajiriwa  na makampuni hayo pamoja na kuahidiwa mamilioni ya pesa.Akiwa Phillips Exeter Academy,  Zuckerberg alishinda tuzo mbalimbali katika masomo ya sayansi
(hesabu, astronomy na fizikia) ambapo alihitimu mwaka 2002 na kujiunga na chuo kikuu maarufu duniani cha Havard.

Akiwa Harvard

Wakati akianza masomo Harvard, tayari alikuwa ameshajipatia umaarufu mkubwa kama ‘programa mwenye kipaji’. Alisoma saikolojia na sayansi ya kompyuta.
Katika mwaka wa kwanza wa masomo, aliandika programu aliyoiita CourseMatch, iliyoruhusu watumiaji kufanya uchaguzi wa madarasa ya kusomea na kuanzisha vikundi vya kujisomea pamoja.
Akiwa mwaka wa pili  alianzisha programu nyingine ambayo awali aliita Facemash, ambayo iliwawezesha wanafunzi kumchagua mtu mwenye sura nzuri kutokana na picha mbalimbali. Kutokana na mwanafunzi mwenzake aliyekuwa akiishi na Zuckerberg
wakati huo, Arie Hasit, anasema kwamba alitengeneza programu hiyo kimasihara.
Anasema walikuwa  na vitabu vilivyoitwa Face Books, vilivyohusisha majina  na picha ya kila mmoja aliyeishi katika mabweni ya wanafunzi.
“Awali, alijenga mtandao huo na kuweka picha mbili tu, au picha mbili za wanaume  na picha mbili za wanawake. Waliotembelea mtandao huo walikuwa na hiyari ya kuchagua ni nani alikuwa mzuri kuliko wengine.
Alitumia maarifa yake ya sayansi ya kompyuta vizuri kwa kuingia katika mtandao wa usalama wa Chuo Kikuu cha Harvard na kunakili picha kutoka kwenyevitambulisho vya wanafunzi wenzake vilivyokuwa vikitumiwa katika mabweni ili kuuboresha mtandao wake wa Facemash. Mtandao huu ulikuwa wazi kwa siku za mwishoni mwa wiki, lakini Jumatatu asubuhi chuo kilikuwa kinaufunga kwa sababu umaarufu wake ulikuwa unafanya mtandao wa chuo kuelemewa kutokana na wanafunzi wengi kuupenda.
Aidha, wanafunzi wengi walilalamika kwamba  picha zao zilikuwa zikitumiwa bila idhini. Mtandao wa Facemash ulianza kufanya kazi Oktoba 28, 2003, na ulifungwa siku chache baadaye na uongozi wa Harvard kuupiga marufuku. 
Zuckerberg alifunguliwa mashitaka ya kukiuka masuala ya usalama, kukiuka hakimiliki na kukiuka uhuru wa mtu binafsi, kwa kuiba picha za wanafunzi wenzake alizotumia kuutangaza mtandao wake. Aidha, alifukuzwa katika Chuo Kikuu cha Harvard kutokana na kitendo hicho.....

Makala hii itaendelea toleo 
lijalo

No comments:

Post a Comment