Showing posts with label H. Show all posts
Showing posts with label H. Show all posts

Friday, October 7, 2016

HISTORIA FUPI YA SCORPION MTOA MACHO


Alivyokuwa mdogo alikataa kusoma, mzazi alishafariki siku nyingi na alikuwa akilelewa na mama yake mdogo maeneo ya Yombo buza.

Alishawahi kufungwa jela japo haijajulikana alikosa nini, na jina lake kamili ni Salum Njwope na jina hilo nila babu yake. Yeye ni mwenyeji wa mkoa wa Shinyanga. Kwa mujibu wa mama yake mdogo anasema Scorpio alipokua akitoka nyumbani usiku saa mbili anamuaga mama yake mdogo huyo kuwa anakwenda kwenye kazi ya ubaunsa katika club kumbe mwenzie alikuwa anaenda Buguruni kuibia watu mpaka asubuhi ndio anarudi nyumbani.

Pia scorpion ashawahi kushiriki katika shindano lililojulikana kama Dume Challenge kama miaka mitatu iliyopita na aliibuka mshindi. Napia alianza mafunzo ya kucheza caret tangu akiwa mdogo sana napia ni mtu mwenye nguvu za kuzaliwa nazo.

Kuna kipindi aliondoka nyumbani kwao kwa muda mrefu mama yake mdogo anadai alikuwa hajui yuko wapi mpaka baadae aliporudi mwenyewe nyumbani.

Amekamatwa na Polisi baada ya kutuhumiwa kumjeruhi mkazi mmoja wa Dar es Salaam eneo la Buguruni kwa kumng’oa macho katika kitendo kilichoelezwa kuwa ni wizi wa fedha.

Salum Mrisho kijana aliyetolewa macho akiongea na vyombo vya habari, pembeni yake RC Makonda

Monday, October 3, 2016

Wamachinga Manispaa ya Bukoba bado hali tete..

  NA YEGESA MABALA-BUKOBA

Wafanyabiashara ndogondogo  almaarufu kama wamachinga katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wameiomba Serikali  kupitia  Manispaa ya Bukoba  kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika eneo jipya la machinjio ya zamani ambapo wamehamishiwa kutoka katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maeneo ya Shaburidini,  maeneo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera(Government) maarufu kama Uganda Road  pamoja  na maeneo tofautitofauti  ya Manispaa hiyo ya Bukoba Mkoani Kagera.
Kauli hiyo ilitolewa na baadhi ya wafanyabiashara hizo ambapo ni pamoja na Bi: HUSNA MOHAMED,Respikius Salatieli na mwingine aliye tambulika kwa majina ya Hashimu Mohamedi wote wakiwa wafanyabiashara wa soko hilo jipya la machinjioni barabara ya Kashozi iendayo Migera Katika Manispaa hiyo ya Bukoba .
Wafanyabiashara  hao wamesema kuwa changamoto kubwa ambayo inawakabili kwa sasa ni pamoja na kutokuwepo kwa ulinzi wa kutosha katika soko hilo ambapo mali zao walisema kuwa haziko katika usalama, muda wote wanawaza pa kuzipeleka wapi pindi wanapofunga na kuondoka kwenda majumbanikwao ambapo wamesema  kuwa ulinzi katika eneo lao hilo unahitajika ili wawe wanaacha biashara zao na kurejea majumbani kwao pasipo kuwa na mashaka yoyote juu ya biashara zao hizo .
Walisema pia Halmashauri ya manispaa hiyo inatakiwa kuwasimamia katika kufanya biashara hiyo kutokana na baadhi ya wamachinga hao kuwa katika vikundi viwili ambavyo ni pamoja na kikundi cha kwanza kushindwa kupanga bidhaa zao ndani ya soko hilo ambapo walipewa eneo na kujenga vibanda lakini cha kushangaza baadhi ya wamachinga wenzao wanashindwa kupanga biashara zao na kuamua kupanga bidhaa hizo mbele kwa kutandaza chini hali ambayo pia wanalalamikiana wao wenyewe katika kile ambacho walisema wanazibiana riziki kw akuwa wateja walio wengi ni wapiti njia na hivyo wanakomea mbele kwa walio tandaza chini na waliomo ndani kushindwa kufikiwa na wateja hao. Hata hivyo Machinga hao walizidi kusisitizakwa kuiomba Serikali kuhakikisha inawaondoa pia wafanyabiashara hao ndogondogo ambao wapo katika maeneo ya stendi Kuu ya mabasi kwa kuwa wameanza kurejea katika maeneo hayo ambayo waliamuliwa kuondoka  kwani kuna huduma zingine ambazo zinahitajika katika soko hilo ambapo zinakosekana kutoka na baadhi ya machinga hao kuwa katika eneo hilo la stendi ya mabasi na hivyo kufanya wanunuzi kutoka eneo hilo na kwenda kutafuta eneo jingine na hivyo kuiomba Serikali kulishughulikia suala hilo.
Kadhalika walisema kuwa eneo hilo ambalo wanafanyia biashara hiyo hawana  uongozi ambao pengine wangeweza kuwasilisha kero zao na walisema kuwa inakuwa vigumu sana katika kwenda kwa pamoja kuwasilisha matatizo yao katika uongozi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo jambo ambalo pia bado ni changamoto katika kupata hatima ya biashara zao. Hata hivyo Gazeti hili la HAMASA lilifika katika viwanjavya machinga hao mnamo mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Diwani wa kata ya Kahororo ambae pia ni Meya wa Manispaa ya Bukoba Mhe: Chief Kalumuna aliwaambia wamachinga hao kuwa matatizo yao hayo yote ambayo yanawakabili yapo mbioni kutatuliwa  na kuwataka machinga hao kuwa wavumilivu pia Serikali ya Mkoa huo wa Kagera kupitia Manispaa hiyo inatambua umuhimu wa wafanyabiashara hao .
Vilevile alipokuwa akiongea nao wamachinga waliweza kumtambulisha uongozi wao mpya walioamua kuuchagua baada ya kuona barua yao ya kuomba uongozi kuchelewa kujibiwa. HAMASA ilifanya mahojiano mafupi na Mwenyekiti aliyechaguliwa na kusema, “Tuliandika barua ya maombi kuhusu uongozi wa soko la machinjioni kwa mtendaji kata Kashai wakaomba tusubiri, baada ya kuchelewa na changamoto kuwa nyingi tukakubaliana kuchagua uongozi wa muda siku ya taehe 25 mwezi huu ambapo mwenyekiti ni mimi Leonidas Kalyamtima, katibu ni Jovonati Clemence na muweka hadhina ni Husna Mohamed” Alimaliza.
Kwa upande wa Meya aliwaambia wamachinga kama wataridhia hao ndo wawe viongozi wao basi wao hawana tatizo, uongozi huo utathibitishwa siku ya kikao rasmi ambacho bado hakijafanyika.










UTALII WA UTAMADUNI MKOANI KAGERA

Hivi vitu pichani ni baadhi ni vya kiutamaduni wa Mhaya ambapo vinapatikana Makumbusho ya Kagera (Kagera Museum)
NA FRANK JOHNSON
Kwa Tanzania,kabila la wamasai ndio pekee linalonufaika na Utalii wa utamaduni, ni utalii ambao mtu anaenda sehemu moja kwenda nyingine kujifunza au kuona mambo ya kitamaduni ya jamii husika kama maisha ya watu,ngoma,chakula,mila na desturi,mtalii anaweza kwenda kuona jamii husika kwenye makazi yao au kwenda kwenye nyumba au sehemu zilizohifadhiwa vitu mbalimbali vya kumbukumbu vilivyotumiwa na jamii husika au ambavyo vinaendelea kutumiwa sasa mfano vikapu,mkuki nakadhalika. Kwa nchi zinazoendelea huu utalii umekuwa mpya kwao lakini utalii unatumiwa na nchi zilizoendelea kama Ujerumani,Uingereza na Marekani na unaingizia serikali mapato makubwa.Mkoa uliopakana na nchi nyingi zaidi Tanzania (Mkoa wa Kagera) umejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo pia utamaduni ambao tukifanikiwa na kuutangaza tutapata wageni wengi sana kuja kuona utamaduni na utaingizia jamii mapato na kupunguza umaskini. Wamasai kutokana na kufanikiwa kuutangaza utamaduni wao,wageni wengi wanaokuja kutembea Tanzania uenda kujifunza na kuwatembeleana kununua vitu mbalimbali vinavyotengenezwa na wamasai. Familia za kimasai zinanufaika sana na utalii wa kiutamaduni na wanaingiza pesa nyingi sana ,wengine hufanikiwa kuingiza hadi sh. 40,000 kwa siku  kutokana na utalii huu wa kiutamaduni.
Utalii wa kiutamaduni una nafasi kubwa sana ya kutoa ajira nyingi na kuingiza kipato kwa mkoa wa Kagera na mikoa mingine ya kanda ya ziwa na kupunguza umaskini uliopo. Mikoa ya kanda ya ziwa imetajwa kwenye ripoti ya serikali kama mikoa duni zaidi japo ina fursa nyingi lakini wananchi wanashindwa kuzitumia sababu ya kukosa elimu.
Mambo ambayo mkoa wa Kagera wanaweza kufanya kutangaza utalii wa kiutamaduni kwanza kutangaza ngoma za asili za makabila mbalimbali yanayopatikana mkoani Kagera,wasanii kama Maua na Saida wamejitaidi sana kutangaza utalii wa ngoma na walifanikiwa kuteka soko la Taanzania na nje ya nchi hivyo inaonesha ni kiasi gani utalii wa kiutamaduni wa mkoa wa Kagera unavyokubalika.
Pili utamaduni wa kumenya ndizi, wageni wengi hasawazungu hawajui jinsi ya kumenya ndizi na huwa wanashangaa mtu anavyoweza kumenya ndizi kwa haraka,kama tukiweza kutangaza utamaduni huu wa kumenya ndizi,wageni wengi watakuja kujifunza kwenye familia mbalimbali namna ya kumenya ndizi na wananchi watanufaika kwa kuongeza kipato na mkoa pia utanufaika.
Tatu mkoa wa Kagera ili kukuza na kutangaza utalii wa kiutamaduni,kila wilaya au mkoa uwe unaandaa siku ya utamaduni na kualika watu mbalimbali kuja kuona utamaduni wa sehemu husika, hii itasaidia kutanga utalii wa kiutamaduni na jamiiitanufaika sana kwa mapato.Wilaya ya Karagwe wamefanikiwa kwa hili kuandaa siku ya utamaduni wa wanyambo na wamefanikiwa kutangaza utalii wao, ni vizuri jitihada zikiendelea za kutangaza utalii huu wa utamaduni.
 Nne mkoa wa Kagera ili kutangaza utalii wa utamaduni nashauri watangaze zaidi nyumba au sehemu zinazohifadhi mambo ya utamaduni, kwa muda mrefu kumekuwa nasehemu zinazotunza mambo ya kale lakini kumekuwa hakuna jitihada kubwa kutangaza hizi sehemu. Serikali ya mkoa inaweza kunufaika sana na utalii huu kama jitihada zikiwekwa za kutangaza.Mwisho ili kupunguza umasikini mkoa wa Kagera hatuna budi kutangaza utalii huu wa utamaduni,mkoa umebahatika sana kuwa na vivutio vingi vya asili na utamaduni ikiwemo pia nyumba za asili na historia ya utamaduni wa makabila mbalimbali yanayopatikana mkoa wa Kagera. Ni wakati sasa wa kutumia fursa hizi ili kunufaika nazo na kipato kwa wananchi kiweze kukua.
   



Friday, September 23, 2016

POLISI YASAMBARATISHA MKUTANO WA UKAWA KAGERA


Polisi yasema hakuna taarifa za mkutano huo, yawataka kufuata waathiriwa majumbani.
Akizungumza na watu takribani sabini waliokuwa wamesubiri viongozi na wageni taifa kuwasili mjini Bukoba katika viwanja vya shule ya msingi Kashai, afisa upelelezi wa polisi wilaya ya Bukoba, amesema kuwa wameshatoa maelekezo kuwa wafanye mkutano wa ndani, na kama ni kuzungumza na waathiriwa wa tetemeko, wanatakiwa kuwazungukia kwenye maeneo yao.
Awali, Mh. Wilifred Muganyizi Lwakatare, aliwaalika wananchi kuudhuria mkutano huo, wakiwasihi kumuunga mkono kuuliza maswali kwa mwakilishi wa mkuu wa wilaya ambaye angejifika mkutanoni hapo.

Tuesday, September 20, 2016

Taarifa ya TUSHIRIKISHANE kwenye gazeti la HAMASA

Muonekano wake kabla gazeti halijawa printed


Mbunge wa Bukoba Mjini (katikati), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media kwa pamoja wakisaini 'MoU
'

 Semina ikiendelea


Washiriki wa semina katika Picha ya pamoja



Hii ni taarifa rasmi iliyochapishwa kwenye Toleo la Pili la Gazeti la Hamasa
Jamii Media, waendeshaji wa mtandao maarufu kwa JamiiForums walikuwa mjini Bukoba kwa siku tatu mfululizo kuanzia Tarehe 3 hadi 5 Agosti, 2016 kwa ziara maalum ya uzinduzi wa Mradi uitwao Tushirikishane.
Mradi huo ambao upo katika hatua ya majaribio una malengo ya kuwasaidia viongozi wa kuchaguliwa na wananchi hususani wabunge kutekeleza ahadi walizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita kwa urahisi. Pia mfumo shirikishi unaotumika katika kuendesha Mradi wa Tushirikishane utasaidia Halmashauri kuboresha na kutoa huduma za jamii kwa ufanisi zaidi.
Akiongea mbele la Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media na Mwanzilishi-Mwenza wa mtandao wa JamiiForums, Ndg. Maxence Melo aliwashukuru viongozi wa Manispaa ya Bukoba, Madiwani na Mbunge Jimbo la Bukoba Mjini kwa kuupokea mradi wa Tushirikishane na kuonyesha utayari wa hali ya juu katika kushiriki utekelezaji wake.
Aliongeza kuwa, Tushirikishane itatekelezwa katika Majimbo Sita(6) na Jimbo la Bukoba Mjini limekuwa la kwanza kuingia katika hatua ya utekelezaji.
Naye Mbunge wa Bukoba Mjini, Mh. Wilfred Lwakatare alizisifu jitihada za Jamii Media katika kuchochea uwajibikaji hususani kwenye sekta ya umma nchini Tanzania. Aliupongeza ubunifu na dhima iliyomo ndani ya mradi wa Tushirikishane na kuyafananisha maudhui yake na nadharia ya “Usimamizi Lazimishi”
Katika warsha hii, washiriki walikuwa ni kutoka makundi yanayowakilisha wadau wakuu wa mradi; ambayo ni wananchi/wapigakura, viongozi wa kuchaguliwa na uongozi wa Halmashauri wamepata kujua malengo, muundo wa mradi, wajibu wa wadau na jinsi ya kushiriki katika hatua na shughuli mbalimbali za mradi. Pamoja na shughuli hizo, yako matukio mengine makuu mawili yalitendekeka sambamba na warsha hii katika kuelekea kwenye utekelezaji wa mradi.
Washiriki walipata kupitia ahadi zilizotolewa na mgombea aliyeshinda kiti cha Ubunge, jimbo la Bukoba Mjini na kuchagua ahadi kuu tatu kwa umuhimu zinazoweza kutekelezeka ndani ya miezi tisa toka sasa.
Ahadi zilizochaguliwa ni fungu la kwanza linajumuhisha Ujenzi wa Kituo cha Mabasi Kyakailabwa, ujenzi wa Soko-Kuu la Bukoba na soko la Kashai, namba mbili ni kuwawezesha vijana na akinamama kujiajiri kwa kuwapa mikopo ya riba nafuu na mwisho ni kurasimisha makazi na maeneo mapya.
Pamoja na vipaumbele hivi, Mh. Lwakatare na Madiwani walikubaliana kuwahamasisha wakazi wa Jimbo la Bukoba Mjini kujiunga na mifuko ya Bima ya Afya. Suala hili limekubalika kuwa mtambuka na hivyo litakuwa mada ya kudumu katika mikutano ya hadhara na ziara za viongozi.
Warsha ya Tushirikishane ilienda mbali zaidi kwa kuandaaa Mpango-Kazi wa utekelezaji wa ahadi zilizochaguliwa kutekelezwa chini ya usimamizi wa mradi. Ili kuhakikisha pande zote zinazohusika katika Mradi zinatekeleza makubaliano, randama (Memorandum of Understanding) ilisainiwa kati ya Ndugu Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media ambaye atatambulika kama msimamizi na muendeshaji wa mradi, Mh. Wilfred Lwakatare Mbunge Jimbo la Bukoba Mjini - mhusika mkuu katika utekelezaji wa ahadi, na Mstahiki Meya, Chief Karumuna kwa niaba ya Baraza la Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba ambalo lina jukumu la kuhakikisha huduma za jamii na Sheria ndogondogo zinaboreshwa.
Jamii Media pia ilimtangaza Mhadhiri Happiness Essau na kumuwezesha kwa kumpatia vitendea kazi vitakachomuwezesha kufanya kazi za Afisa Mawasiliano wa Mradi katika Jimbo la Bukoba Mjini kwa ufanisi. Mhadhiri Happiness atakuwa na jukumu la kukusanya na kusambaza habari zilizothibitishwa juu ya maendeleo ya utekelezaji wa Mpango-Kazi.
Njia zitakazotumika kupashana habari ni pamoja na mitandao ya kiganjani (WhatsApp, Telegram), uzi maalumu kwenye tovuti ya JamiiForums.com, makala kupitia FikraPevu.com, kurasa za mitandao ya Twitter, Facebook, Instagram zinazomilikiwa na Jamii Media na kupitia vyombo vingine vya habari.
Gazeti lako pendwa la HAMASA ni mdau aliyeidhinishwa kutoa taarifa rasmi juu ya maendeleo ya mradi wa Tushirikishane kwa Jimbo la Bukoba Mjini. Wananchi na wadau wenye kiu ya kuiona Bukoba ikipiga hatua kimaendeleo wanakaribishwa kuitumia HAMASA kuonyesha jinsi gani Tushirikishane inaweza kupanuliwa kwa faida kubwa zaidi.
Description: https://ssl.gstatic.com/ui/v1/icons/mail/images/cleardot.gif



- MWISHO -

Historia ya Karagwe kuandikwa upya

Akizungumza na Hamasa mwanzilishi wa siku ya Utamaduni wa Wanyambo ‘alifunguka’  kama ifuatavyo;-

MUANDAAJI - Kazi hii ya kuunda upya historia ya karagwe  lilikuwa wazo la watu wawili ambao ni mimi mwenyewe, Bullet Straton Ruhinda (Sociologist/ Anthropologist) na Edward Frontline Ruhinda (Environmental Engineer). Wazo lilikuwa ni kuandika historia hii kwa kutumia mbinu yaani kutumia mtazamo kwa namna ya kuwapitia wazee na watu wote wenye historia ya Karagwe ili kuweza kuiweka kwenye kumbukumbu kwa kizazi kijacho”. Pia ababu ya wazo hili ilikuwa ni kwamba Karagwe inayo historia kongwe sana hapa Tanzania ukiondoa historia ya ukanda wa Pwani hasa Zanzibar na Kilwa, Karagwe ilifuata kwa ukongwe. Pia Karagwe ni moja kati ya falme  katikaAfrika ya Mashariki hasa  kwa Tanzania..Historia ya Karagwe ukiondoa Prof Katoke na Mzee Pesha, imeandikwa zaidi na wageni wakiaongozwa na Speke, Prof. Birgita Farelius na wengineo. Katika kuikusanya historia hii kulikuwa na mpango wakufanya utamaduni wa Karagwe na Kagera kwa ujumla kuwa chanzo cha utalii. Hii ni pamoja kufufua makumbusho kama Ikulu za Karagwe na kuzifanya kuwa vivutio vya watalii.Vilevile kulikuwepo mpango wa kuzitambua na kuzikusanya mali za kale za karagwe na kuzihifadhi vizuri kwa kizazi kijacho. Baadhi ya mali za kale hizo zipo mikononi mwa watu na nyingine zipo serikalini ila utunzaji wake sio mzuri. Zipo sehemu kama Mtagata, na maeneo ya maziko ya Bakama ambayo yameanza kuharibika yanatakiwa kutunzwa na kuhifadhiwa na bado Kuna mchakato wa kushirikiana na serikali na wadau wengine ambapo tuliona ni vema kuanzisha siku ya utamaduni ambayo itakuwa inaazimishwa kila tarehe 21 Mei ya kila mwaka na huu ni mwaka wa pili mfululizo kuanzia mwaka 2015. Tarehe hiyo kila mwaka kunakuwa na maonyesho ya kitamaduni  na mali za kale toka maeneo mbalimbali ya Karagwe. Kwa kweli mwitikio ni mzuri sana kama  nitakumbuka vizuri mwaka jana watu walisafiri toka Karagwe nzima kuja kuazimisha siku ya tarehe 21 Mei. Mwaka huu imekuwa na ufanisi mkubwa zaidi, watu wamesafiri toka mikoani kuja kushuhudia.. Pia mwaka huu kulikuwa na wawakilishi kutoka nje ya nchi. Ufalme wa Bunyoro  pia falme jirani kama Kianja(Kamachumu), Busubi(Biharamulo) na Bugufi(Ngara). Wote hao wamekuja kwa gharama zao.
Katika harakati zetu tumejaribu kupitia falme za zamani kuangalia jinsi ya kuifanya historia ya Kagera iwe katika nyaraka. Baadhi ya falme tumepitia ni pamoja na Kianja, Kyamutwara na Bugufi.

Aliendelea kwa kusema kuzungumzumzia upande wa uwezeshaji wa Tamasha ambapo alisema, “Kwa asilimia kubwa naliwezesha mimi, wananchi wanachangia kidogo, kwa upande wa Serikali imesaidia sana katika kuweka mazingira ya kufanyika kwa Tamasha”.
Aidha ametoa shukrani kwa Redio za kijamii kama Fadeco na Karagwe kwa mchango wao wa matangazo ya bure kuhusu Tamasha hilo.walipendekeza baadae iwe ya kimkoa. Ndio maana tulifikia hatua ya kwenda katika Falme nyingine kama Bugufi, Kianja na Busubi. Mwakani tamasha linategemea kuhusisha watu wengi zaidi toka mkoani Kagera maana Kagera ni moja na utamaduni unakaribiana sana.


Monday, September 19, 2016

"Tetemeko halijaletwa na Serikali"-Rais Magufuli




Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amepokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na tetemoko la ardhi lililotokea katika Mkoa wa Kagera na mikoa jirani ya Mwanza, Geita na Mara kutoka kwa Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Ikulu DSM.

Pamoja na kupokea taarifa hiyo Rais Magufuli amepokea mchango wa fedha taslimu kiasi cha Dola za Kimarekani laki mbili (USD-200,000/-) sawa na takribani Shilingi za Kitanzania Milioni Mia nne na therathini na saba (Tshs-437,000,000/-) kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni na pia amepokea taarifa ya mchango wa mabati, blanketi na magodoro vyenye thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni 115 kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.

Katika taarifa yake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 17, majeruhi 440, nyumba 2063 zimeanguka, nyumba 14,081 zipo katika hali hatarishi na nyumba 9,471 zimepata uharibifu mdogo, huku watu 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

Mhe. Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kupeleka chakula, huduma za matibabu na hifadhi za dharura kwa waathirika na pia inaratibu ukusanyaji wa michango kutoka sehemu mbalimbali ambapo mpaka sasa kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni tatu nukta sita (Tshs Bilioni 3.6) zimepatikana.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya maafa na michango kwa ajili ya waathirika wa maafa hayo, Rais Magufuli amewashukuru wote waliojitoa kusaidia waathirika wakiwemo Marais Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Mhe. Uhuru Kenyatta wa Kenya na Paul Kagame wa Rwanda ambao wamempigia simu za kumpa pole na tayari wametoa misaada yao, na pia nchi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara, watumishi wa umma na watu binafsi na amesema michango hiyo ina umuhimu mkubwa katika kukabiliana na athari za maafa haya.

Dkt. Magufuli ametoa wito kwa Watanzania na wote walioguswa na maafa haya kuendelea kutoa misaada kwa waathirika kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, huku akionya na kuvitaka vyombo vya dola kuwafuatilia watu wanaotaka kutumia maafa haya kukusanya michango kwa lengo la kujinufaisha.

Rais Magufuli amebainisha kuwa Serikali itahakikisha inarekebisha miundombinu iliyoharibika zikiwemo shule, vituo vya matibabu, barabara na huduma nyingine za kijamii na pia ametaka wananchi waliokumbwa na madhara ya tetemeko hususani nyumba zilizobomoka, wajipange kurekebisha nyumba zao kwa kuwa Serikali pekee yake haitaweza kujenga nyumba zote zilizobomoka.

Aidha, Rais Magufuli amewasihi Watanzania kuwapuuza watu wanaotaka kutumia maafa haya kueneza uchonganishi na chuki dhidi ya Serikali na ameweka wazi kuwa mpaka sasa hakuna teknolojia ya kutabiri kutokea kwa tetemeko la ardhi na kwamba tetemeko hili halikuletwa na Serikali.

Dkt. Magufuli amesema hata mataifa makubwa yenye maendeleo makubwa ya uchumi na teknolojia yanakumbwa na tetemeko la ardhi na kusababisha vifo vya idadi kubwa ya wananchi na uharibifu mkubwa wa mali.

"Nilikuwa najaribu kuangalia kwa mfano nchi kama China kwenye mwaka 2014 watu 617 walipoteza maisha, Mwaka 2013 walipoteza watu 193, Mwaka 2010 walipoteza watu 2,998 Mwaka 2008 China ilipoteza watu 98,712.

Ukijaribu kuangalia Japan, nchi ambayo imeendelea na ina utaalamu wa hali ya juu sana, kwenye mwaka 2016 tarehe 14 mwezi wa nne ilipoteza watu 6, baada ya siku mbili tarehe 16 mwezi wa nne 2016 tetemeko likatokea tena na likaua watu 35, mwaka 2012 likaua watu 3, mwaka 2011 likaua watu 15,904 mwaka 2008 likaua watu 12, mwaka 2007 likaua watu 11, mwaka 2004 likaua watu 40, mwaka 1923 liliua watu 142,800 na hiyo ni Japan. Amesisitiza Rais Magufuli.

Shughuli ya kupokea taarifa ya Waziri Mkuu na michango kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera na Mikoa jirani imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt Suzan Kolimba, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Balozi wa Uganda nchini Tanzania Mhe. Dorothy Hyuha na Naibu Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mhe. Boniface Muhia.




Chanzo: IPP Media

TAARIFA YA MKUU WA MKOA KUHUSU HATUA ZINAZOENDELEA KUCHUKULIWA NA SERIKALI KUKABILIANA NA JANGA LA TETEMEKO LA ARDHI KAGERASEPTEMBA 17, 2016.

Ndugu Waandishi wa Habari, Kama mnavyojua Mkoa wetu wa Kagera ulipatwa na janga la tetemeko la ardhi tarehe 10.09.2016, kutokana na janga hilo Serikali kwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wananchi tulichukua hatua za haraka ili kukabiliana na janga hilo, na leo nimewaiteni ili niwape taarifa tulizochukua mpaka sasa ili kunusuru wahanga waliokumbwa na janga hilo katika mkoa wetu.Ndugu Waandishi wa Habari, Mara baada ya tetemeko hilo kutokea, kwenye mkoa mzima wananchi waliojeruhiwa ni 440 na kati ya majeruhi hao 253 walifika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, pia majeruhi 151 walilazwa ambapo majeruhi 113 tayari wametibiwa na kuruhusiwa. Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wamebaki majeruhi 38 na kati ya hao majeruhi 23 walihitaji huduma za upasuaji na tayari wote wameishafanyiwa upasuaji huo na wanaendelea vizuri.Aidha, majeruhi 187 walifika katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Kagera na walitibiwa na kuruhusiwa na kufikia jumla ya majeruhi ambao walitibiwa na kuruhusiwa 412 kati ya 440. Vifo vilivyosababishwa na janga hilo ni 17 hadi kufikia siku ya leo.Ndugu Waandishi wa Habari, Tetemeko la ardhi mkoani Kagera hadi sasa limesababisha nyumba 2,063 kuanguka, Nyumba zenye uharibifu hatarishi 14,081. Nyumba zenye uharibifu mdogo 9,471. Aidha, wananchi walioathirika na wanahitaji misaada ili kurudi katika mfumo wa kawaida wa maisha yao ni 126,315Ndugu Waandishi wa Habari, Kufuatia madhara hayo yaliyojitokeza mahitaji mablimbali ya kibinadamu ya muda mfupi na muda mrefu yanahitajika. Mahitajihayo ni madawa na vifaa tiba, Chakula, Vifaa vya Ujenzi kama simenti, misumari, mabati na mbao.Hadi kufikia sasa Kamati ya maafa ya Mkoa wa Kagera tayari imepokea msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwa ni Madawa na vifaa tiba, Chakula, (Matrubali, mahema mashuka na mablanketi), vifaa vya ujenzi kama mbao, misumari, mabati na simenti vyenye gharama ya zaidi ya shilingi milioni 431,715,800/=Ndugu Waandishi wa Habari, Kwa upande wa dawa na vifaa tiba wadau mbalimbali pamoja na Serikali wameweza kuchangia dawa na vifaa tiba vya kutosha hadi sasa hakuna upungufu wa dawa na vifaa tiba katika hospitali zetu.Aidha kwa mahitaji ya haraka tayari Kamati ya mkoa imegawa chakula kwa wahanga katika mkoa mzima kama ifuatavyo: unga wa sembe kilo 3750, mchele kilo 1850, sukari tani 6.5, maharage kilo 3470, bisukuti katoni 2600, na maji ya kunywa katoni 615. Pia wahanga wamegawiwa mahitaji muhimu kama mablanketi 480 mahema 119 na matrubali 320. Huo ulikuwa ugawaji wa mahitaji wa awali na kamati zinaendelea kugawa mahitaji hayo katika maeneo yaliyoathirika na yataendelea kugawiwa kadri tunavyopokea misaada ya mahitaji hayo.Ndugu Waandishi wa Habari, Napenda sasa kutoa taarifa ya michango mbalimbali ambayo tayari tumeipokea kutoka kwa wadau mbalimbali; Katika Harambee tuliyoifanya jana tarehe 16/09/2016 tuliweza kukusanya kiasi cha fedha taslimu pamoja na hundi 7,800,000/=, ahadi ya fedha na vifaa ni shilingi milioni 770,502,000/= kama wadau hawa wote watatoa michango yao jumla tutakuwa tumepata shilingi milioni 778,302,000/=
Kupitia Akaunti yetu iliyoko Benki ya CRDB inayojulikana kama “KAMATI YA MAAFA KAGERA CRDB BUKOBA” Akaunti Namba 0152225617300 tayari tumekusanya kiasi cha shilingi 623, 624,200/=. Aidha, baada ya Mhe, Waziri Mkuu kuzindua namba za simu za kuchangia maafa Kagera tayari wananchi wameanza kuchangia michango yao kupitia namba hizo ambazo ni (M.PESA 0768 196 669), (AIRTEL MONEY 0682 950 009), (TIGO PESA 0718 069 616).Ndugu Waandishi wa Habari, Napenda kuwashukuru wananchi na wadau mbalimbali wote wanaoendelea kujitoa kwa kuchangia maafa yaliyotupata katika Mkoa wetu wa Kagera pia natoa wito kwa kila Mwananchi, Mdau, Taasisi mbalimbali ambao hawajachangia kuendelea kuchangia kupitia akaunti ya benki na namba za simu zilizotajwa hapo juu kwani mahitaji bado ni makubwa sana.
Ndugu Waandishi wa Habari, Kabla ya kuhitimisha naomba kueleza mkakati wa Kamati yangu tunaondelea nao kuwa ni kugawa mahitaji mbalimbali kwa wahanga kadri tunavyoupokea. Pia wajumbe wote wa Kamati wamegawanywa katika maeneo mbalimbali ya mkoa yaliyopatwa na majanga ili kusimamia zoezi la kugawa mahitaji na kuhakikisha hakuna mwananchi aliyeathirika na janga la tetemeko ameachwa bila kusaidiwa.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mwisho napenda kuwashukuru Waandishi wote wa Habari pamoja na vyombo vyao vya habari kwa kufanya kazi yao kwa ushirikiano mkubwa na Kamati yangu kwa kuwafikishia habari wananchi habari muhimu kuhusu janga lililotupata mkoa wetu.
MWISHO