Monday, October 3, 2016

Tajirika kupitia Ufugaji wa Nyuki kwa mtindo wa kisasa

NA FRANK JOHNSON

Kufuga nyuki na kuzalisha asali kwa mtindo wa kisasa kwa kujenga nyumba ya nyuki inamwezesha mfugaji wa nyuki kuongeza uzalishaji wa asali na hatimaye kupata kipato zaidi.Ufugaji wa nyuki ni kazi ambayo imekuwepo kwa karne nyingi sana.Shughuli ya ufugaji wa nyuki nchini Tanzania hasa katika mkoa wa Tabora ambao ni maarufu kwa uzalishaji wa asali ilianza kutambulika rasmi tangu mwaka 1884, wakoloni kama Rebman na craft walipofika katika eneo hilo. Kwa kutambua faida za ufugaji wa nyuki, Mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali mstaafu  Salum Kijuu aliweza kukabidhi mizinga ya nyuki kwa vijana na kina mama wa wilaya ya Karagwe mkoani Kagera ili iwasaidie kufanya kazi hiyo kwa ufanisi  na kuweza kujipatia kipato kizuri. Hivyo kwa kutambua umuhimu wa ufugaji wa nyuki,Gazeti la Hamasa limeamua kutoa elimu hii kwa wafugaji wa nyuki ili waweze kufuga kwa mtindo wa kisasa na kuweza kabisa kuondoa umaskini kwa vijana kupitia ufugaji huu.

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA UFUGAJI WA NYUKI.

NYUMBA YA NYUKI.
Hii ni aina mpya ya ufugaji wa nyuki ambapo unaweza kujenga kibanda au nyumba kisha kuweka mizinga idadi unayohitaji.

SABABU YA KUJENGA NYUMBA AU KIBANDA.
• Ni muhimu kufuga nyuki kwenye kibanda kwa sababu inasaidia kudhibiti wizi wa mizinga pamoja na wanyama wanaokula asali.
• Inarahisisha utunzaji wa mizinga na kuwafanya nyuki wasihame kwenda sehemu nyingine.
• Inasaidia watu wengi kujifunza namna nzuri ya ufugaji wa nyuki, ikiwa ni pamoja na watoto jambo ambalo linafanya shughuli hii kuwa endelevu.
• Uzalishaji unaongezeka, hii ni kwa sababu mizinga inayotumika ni ile ya kibiashara.mzinga 1 unapata asali kilo 30 sawa na lita 20.
• Ufugaji wa aina hii usaidia kuwakinga nyuki dhidi ya majanga kama vile moto na mafuriko.
• Inawaepusha nyuki na usumbufu unaoweza kuwafanya nyuki wasizalishe kwa kiwango kinachotakiwa

AINA YA NYUMBA
Unaweza kujenga nyumba yenye upana wa futi 3 na urefu wa futi 9.Nyumba hii inaweza kuchukua mizinga 50, halikadhalika unaweza kujenga kibanda chenye ukubwa sawa na huo.

ENEO LINALOFAA.

• Ili kuwa na ufanisi mzuri,nyumba hii inafaa kujengwa nje kidogo ya makazi ya watu
• Kusiwe na mifugo
• Iwe sehemu ambayo watoto hawawezi kufika
• Isiwe karibu na njia ambayo watu wanapita mara kwa mara
• Kusiwe na aina ya mimea ambayo nyuki hawapendi.na kuwe na maji karibu.

MAVUNO
Baada ya kujenga nyumba, kuweka mizinga na nyuki kuingia, unaweza kuvuna kwa mara ya kwanza baada ya miezi mitatu (3).Utaweza kupata mavuno mazuri endapo utavuna kabla nyuki na wadudu wengine hawajaanza kula asali.
Ni muhimu kuhakikisha kuwa wadudu waharibifu kama vile sisimizi, mende na wengineo wanadhibitiwa ili kutokuathiri uzalishaji wa asali.
UMUHIMU WA ASALI.

• Asali inatumika kama chakula
• Asali inatumika kama tiba ya magonjwa mbalimbali.
• Asali hutumika kutibu majeraha.
• Ni chanzo kizuri cha mapato.
• Hutumika kutengeneza dawa za binadamu.
• Asali inaweza kuhifadhiwa kwa miaka mingi sana bila kuharibika.Hii inatokana na wingi wa dawa maalumu iliyonayo inayofanya isiharibike

BIDHAA ZITOKANAZO NA ASALI.
• Asali yenyewe.
• Royal Jelly: Hii ni aina ya maziwa
Hakikisha unavuna kitaalamu

yanayotengenezwa na nyuki ambayo hutumika kama tiba

.• Gundi: Hii hutumika kutengeneza bidhaa za aina mbalimbali kulingana na mahitaji ya mtumiaji.

• Nta: Hutumika kutengeneza mishumaa kulainisha nyuzi, kutengeneza dawa ya viatu, mafuta ya kupaka, pamoja na dawa ya ngozi.

Hivo kuna soko kubwa sana la asali kutokana na mahitaji yake, ni jukumu lako mjasiriamali kuwekeza kwenye kufuga nyuki. Mnaweza mkawa kikundi na hatimaye mkashirikiana kufuga nyuki kwa ajili ya kupata asali ili kujikwamua kiuchumi.



No comments:

Post a Comment