Friday, October 7, 2016

HISTORIA FUPI YA SCORPION MTOA MACHO


Alivyokuwa mdogo alikataa kusoma, mzazi alishafariki siku nyingi na alikuwa akilelewa na mama yake mdogo maeneo ya Yombo buza.

Alishawahi kufungwa jela japo haijajulikana alikosa nini, na jina lake kamili ni Salum Njwope na jina hilo nila babu yake. Yeye ni mwenyeji wa mkoa wa Shinyanga. Kwa mujibu wa mama yake mdogo anasema Scorpio alipokua akitoka nyumbani usiku saa mbili anamuaga mama yake mdogo huyo kuwa anakwenda kwenye kazi ya ubaunsa katika club kumbe mwenzie alikuwa anaenda Buguruni kuibia watu mpaka asubuhi ndio anarudi nyumbani.

Pia scorpion ashawahi kushiriki katika shindano lililojulikana kama Dume Challenge kama miaka mitatu iliyopita na aliibuka mshindi. Napia alianza mafunzo ya kucheza caret tangu akiwa mdogo sana napia ni mtu mwenye nguvu za kuzaliwa nazo.

Kuna kipindi aliondoka nyumbani kwao kwa muda mrefu mama yake mdogo anadai alikuwa hajui yuko wapi mpaka baadae aliporudi mwenyewe nyumbani.

Amekamatwa na Polisi baada ya kutuhumiwa kumjeruhi mkazi mmoja wa Dar es Salaam eneo la Buguruni kwa kumng’oa macho katika kitendo kilichoelezwa kuwa ni wizi wa fedha.

Salum Mrisho kijana aliyetolewa macho akiongea na vyombo vya habari, pembeni yake RC Makonda

Monday, October 3, 2016

MFAHAMU MWANZILISHI WA FACEBOOK (SEHEMU YA KWANZA}

NA DIDAS MUGYABUSO
(Kwa msaada wa tovuti mbalimbali)



Mark Elliot Zuckerberg alizaliwa Mei 14, 1984, eneo la White Plains, New York, ni mtoto wa pekee wa kiume na wa pili kuzaliwa kwa mama Karen Zuckerberg, daktari wa  magonjwa ya akili na baba Edward Zuckerberg, daktari wa meno. Yeye na dada zake watatu; Randi, Donna, na Arielle, walikulia Dobbs Ferry, New York. Uwezo wake wa kuandika programu haukuibuka kama miujiza, alianza kuvutiwa na masomo ya kompyuta tangu utotoni, akiwa na miaka 10 alipata kompyuta yake ya kwanza aina ya Quantex 486DX  kipindi hicho ni mwanafunzi wa shule ya kati, akiwa na miaka 12 babayake alimfundisha Lugha ya kikompyuta inayoitwa Atari Basic Programming
miaka ya 1990, aliitumia lugha hiyo kutengeneza mesenja ambayo aliiita ZuckerNet, iliziunganisha kompyuta zote zilizopo nyumbani kwao na ofisi ya babayake ya magonjwa ya meno iliyokuwa jirani na nyumba yao. Babayake aliiweka mesenja kwenye kompyuta yake ya ofisini na mtu wa mapokezi aliweza kumtaarifu  mgonjwa mpya anapoingia ofisini kwa kutumia programu hiyo. Babayake Edward Zuckerberg alikuwa akim’sapoti’ sana mtoto wake, baada ya kugundua ana kitu ndani yake, ilifika kipindi akamkodi mwalimu wa kompyuta ‘software developer’ David Newman ili amfundishe mtoto wake kama mwalimu binafsi. Newman alimwita mwanafunzi wake ‘mwenye akili nyingi’, kiasi kwamba ilikuwa vigumu kumtangulia. Zuckerberg pia alichukua mafunzo ya somo hilo katika Chuo cha Mercy, jirani na nyumbani kwao, alipokuwa bado akisoma ‘high school’. Alifurahia kujifunza programu za kompyuta, hasa vifaa vya mawasiliano na michezo. Pia alipokuwa elimu ya juu ‘High School’ aliandika code na kufanikiwa kutengeneza programu ya kucheza mziki aliyoiita Synapse Media Player kwa ajili ya kucheza miziki iliyo kwenye mfumo wa MP3,programu hiyo ilikuwa na uwezo wa kujua mtumiaji anapendelea miziki ya namna gani na kuweza kumtengenezea mtumiaji ‘playlist’ ya miziki kwa kukisia miziki anayopenda mtumiaji. Makampuni makubwa  ya Teknolojia duniani kama Microsoft na AOL walivutiwa sana na ujio wa programu hiyo ya Synapse Media Player na kila moja ilikuwa ikimshawishi Mark kuwauzia programu hiyo kwa kumtumia ofa nzuri, hata hivyo ‘jiniazi’ huyo alikataa ofa hizo za makampuni hayo mazito duniani, na alikataa ofa ya kushirikiana nao katika kazi. Aliendelea kukataa ofa hizo zilizokuja mara kwa mara za kuajiriwa  na makampuni hayo pamoja na kuahidiwa mamilioni ya pesa.Akiwa Phillips Exeter Academy,  Zuckerberg alishinda tuzo mbalimbali katika masomo ya sayansi
(hesabu, astronomy na fizikia) ambapo alihitimu mwaka 2002 na kujiunga na chuo kikuu maarufu duniani cha Havard.

Akiwa Harvard

Wakati akianza masomo Harvard, tayari alikuwa ameshajipatia umaarufu mkubwa kama ‘programa mwenye kipaji’. Alisoma saikolojia na sayansi ya kompyuta.
Katika mwaka wa kwanza wa masomo, aliandika programu aliyoiita CourseMatch, iliyoruhusu watumiaji kufanya uchaguzi wa madarasa ya kusomea na kuanzisha vikundi vya kujisomea pamoja.
Akiwa mwaka wa pili  alianzisha programu nyingine ambayo awali aliita Facemash, ambayo iliwawezesha wanafunzi kumchagua mtu mwenye sura nzuri kutokana na picha mbalimbali. Kutokana na mwanafunzi mwenzake aliyekuwa akiishi na Zuckerberg
wakati huo, Arie Hasit, anasema kwamba alitengeneza programu hiyo kimasihara.
Anasema walikuwa  na vitabu vilivyoitwa Face Books, vilivyohusisha majina  na picha ya kila mmoja aliyeishi katika mabweni ya wanafunzi.
“Awali, alijenga mtandao huo na kuweka picha mbili tu, au picha mbili za wanaume  na picha mbili za wanawake. Waliotembelea mtandao huo walikuwa na hiyari ya kuchagua ni nani alikuwa mzuri kuliko wengine.
Alitumia maarifa yake ya sayansi ya kompyuta vizuri kwa kuingia katika mtandao wa usalama wa Chuo Kikuu cha Harvard na kunakili picha kutoka kwenyevitambulisho vya wanafunzi wenzake vilivyokuwa vikitumiwa katika mabweni ili kuuboresha mtandao wake wa Facemash. Mtandao huu ulikuwa wazi kwa siku za mwishoni mwa wiki, lakini Jumatatu asubuhi chuo kilikuwa kinaufunga kwa sababu umaarufu wake ulikuwa unafanya mtandao wa chuo kuelemewa kutokana na wanafunzi wengi kuupenda.
Aidha, wanafunzi wengi walilalamika kwamba  picha zao zilikuwa zikitumiwa bila idhini. Mtandao wa Facemash ulianza kufanya kazi Oktoba 28, 2003, na ulifungwa siku chache baadaye na uongozi wa Harvard kuupiga marufuku. 
Zuckerberg alifunguliwa mashitaka ya kukiuka masuala ya usalama, kukiuka hakimiliki na kukiuka uhuru wa mtu binafsi, kwa kuiba picha za wanafunzi wenzake alizotumia kuutangaza mtandao wake. Aidha, alifukuzwa katika Chuo Kikuu cha Harvard kutokana na kitendo hicho.....

Makala hii itaendelea toleo 
lijalo

Tajirika kupitia Ufugaji wa Nyuki kwa mtindo wa kisasa

NA FRANK JOHNSON

Kufuga nyuki na kuzalisha asali kwa mtindo wa kisasa kwa kujenga nyumba ya nyuki inamwezesha mfugaji wa nyuki kuongeza uzalishaji wa asali na hatimaye kupata kipato zaidi.Ufugaji wa nyuki ni kazi ambayo imekuwepo kwa karne nyingi sana.Shughuli ya ufugaji wa nyuki nchini Tanzania hasa katika mkoa wa Tabora ambao ni maarufu kwa uzalishaji wa asali ilianza kutambulika rasmi tangu mwaka 1884, wakoloni kama Rebman na craft walipofika katika eneo hilo. Kwa kutambua faida za ufugaji wa nyuki, Mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali mstaafu  Salum Kijuu aliweza kukabidhi mizinga ya nyuki kwa vijana na kina mama wa wilaya ya Karagwe mkoani Kagera ili iwasaidie kufanya kazi hiyo kwa ufanisi  na kuweza kujipatia kipato kizuri. Hivyo kwa kutambua umuhimu wa ufugaji wa nyuki,Gazeti la Hamasa limeamua kutoa elimu hii kwa wafugaji wa nyuki ili waweze kufuga kwa mtindo wa kisasa na kuweza kabisa kuondoa umaskini kwa vijana kupitia ufugaji huu.

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA UFUGAJI WA NYUKI.

NYUMBA YA NYUKI.
Hii ni aina mpya ya ufugaji wa nyuki ambapo unaweza kujenga kibanda au nyumba kisha kuweka mizinga idadi unayohitaji.

SABABU YA KUJENGA NYUMBA AU KIBANDA.
• Ni muhimu kufuga nyuki kwenye kibanda kwa sababu inasaidia kudhibiti wizi wa mizinga pamoja na wanyama wanaokula asali.
• Inarahisisha utunzaji wa mizinga na kuwafanya nyuki wasihame kwenda sehemu nyingine.
• Inasaidia watu wengi kujifunza namna nzuri ya ufugaji wa nyuki, ikiwa ni pamoja na watoto jambo ambalo linafanya shughuli hii kuwa endelevu.
• Uzalishaji unaongezeka, hii ni kwa sababu mizinga inayotumika ni ile ya kibiashara.mzinga 1 unapata asali kilo 30 sawa na lita 20.
• Ufugaji wa aina hii usaidia kuwakinga nyuki dhidi ya majanga kama vile moto na mafuriko.
• Inawaepusha nyuki na usumbufu unaoweza kuwafanya nyuki wasizalishe kwa kiwango kinachotakiwa

AINA YA NYUMBA
Unaweza kujenga nyumba yenye upana wa futi 3 na urefu wa futi 9.Nyumba hii inaweza kuchukua mizinga 50, halikadhalika unaweza kujenga kibanda chenye ukubwa sawa na huo.

ENEO LINALOFAA.

• Ili kuwa na ufanisi mzuri,nyumba hii inafaa kujengwa nje kidogo ya makazi ya watu
• Kusiwe na mifugo
• Iwe sehemu ambayo watoto hawawezi kufika
• Isiwe karibu na njia ambayo watu wanapita mara kwa mara
• Kusiwe na aina ya mimea ambayo nyuki hawapendi.na kuwe na maji karibu.

MAVUNO
Baada ya kujenga nyumba, kuweka mizinga na nyuki kuingia, unaweza kuvuna kwa mara ya kwanza baada ya miezi mitatu (3).Utaweza kupata mavuno mazuri endapo utavuna kabla nyuki na wadudu wengine hawajaanza kula asali.
Ni muhimu kuhakikisha kuwa wadudu waharibifu kama vile sisimizi, mende na wengineo wanadhibitiwa ili kutokuathiri uzalishaji wa asali.
UMUHIMU WA ASALI.

• Asali inatumika kama chakula
• Asali inatumika kama tiba ya magonjwa mbalimbali.
• Asali hutumika kutibu majeraha.
• Ni chanzo kizuri cha mapato.
• Hutumika kutengeneza dawa za binadamu.
• Asali inaweza kuhifadhiwa kwa miaka mingi sana bila kuharibika.Hii inatokana na wingi wa dawa maalumu iliyonayo inayofanya isiharibike

BIDHAA ZITOKANAZO NA ASALI.
• Asali yenyewe.
• Royal Jelly: Hii ni aina ya maziwa
Hakikisha unavuna kitaalamu

yanayotengenezwa na nyuki ambayo hutumika kama tiba

.• Gundi: Hii hutumika kutengeneza bidhaa za aina mbalimbali kulingana na mahitaji ya mtumiaji.

• Nta: Hutumika kutengeneza mishumaa kulainisha nyuzi, kutengeneza dawa ya viatu, mafuta ya kupaka, pamoja na dawa ya ngozi.

Hivo kuna soko kubwa sana la asali kutokana na mahitaji yake, ni jukumu lako mjasiriamali kuwekeza kwenye kufuga nyuki. Mnaweza mkawa kikundi na hatimaye mkashirikiana kufuga nyuki kwa ajili ya kupata asali ili kujikwamua kiuchumi.



Senene heshima na biashara ya mhaya



HAMASA - KAGERA

Senene  mdudu anayefanana  na panzi ameweza kuwa mdudu wa kuthaminika zaidi katika jamii ya watu wa Mjini Bukoba  kwani amekua zao zuri la biashara vilevile ni chakula cha heshima kwa kabila la Wahaya  .Wadudu hao(Senene) ni wadudu ambao hupatikana kwa msimu na kwa kiasi kikubwa katika maeneo baadhi ya Mkoa wa Kagera na nje ya mkao wa kagera ambao hutegwa na wengine hukamatwa na watu kwa ajili ya kuliwa nyumbani au kwa ajli ya biashara ni moja kati ya biashara iliyowaingizia wakazi wengi wa Mjini Bukoba kutokana na watu wengi kufurahia chakula ya wadudu hao. Senene hupatikana kwa misimu katika mwezi wa 4 na 11 ambapo huonekana  katika maeneo yenye nyasi  ndefu au fupi na watu huanzia hapo kuwakamata wadudu hao, watoto kwa wakubwa hujihusisha na kuwakamata Senene kwajili ya chakula au kwajili ya biashara. Wafanyabiashara mbalimbali wamejikita katika biashara ya senene kwasababu imeonekana kuwa nafaida kibiashara. Senene huitajika kwa kiasi kikubwa  kwa ajili ya biashara kila msimu wafanya biashara huwakamata senene  kwa wingi katika magunia na madiaba, Ili kukamata senene wengi kiasi hicho huhitajika maandalizi  makubwa na ya mda ,Senene kwajili ya biashara hukamatwa  jioni au usiku kwa kutumia taa zenye mwanga mkali  ambazo hutegeshwa kwajili ya kuvutia  senene hao nyakati za usiku pamoja na mabati marefu kwenda juu yaliyoelekezwa kwenye midomo ya madiaba, pia huachiliwa moshi mzito unao vuka kwenda juu ambao ndio humkosesha senene nguvu na kuanguka katika madiaba yaliyo tegeshwa kupitia mabati  senene huvutiwa na mwanga nyakati za jioni na huufwata mwanga huo hivyo ndivyo hujikuta wakiliwa.
Zaidi ya asilimia 10.5% ya wakazi wa Mjini Bukoba kila ifikapo msimu wa senene hujikita na biashara hiyo ya Senene na  huuzwa kwa mifuko midogo au pakiti  au kwa magunia na madiaba kwa fungu la bei ya chini kabisa senene huuzwa shiling 500 pesa ya kitanzania.
Senene ni chakula ya asili ya Muhaya  na hupewa heshima kubwa hasa katika maeneo ya vijijini ambako asili hutokea,wagen rasmi katika famili waliokuja kutoa Mahali au Wazee wenye heshima kubwa  hukalibishwa kwa kupewa  Senene kama heshima ya ujio wa watu hao.

MAKALA: SANAA YA UCHONGAJI

HAMASA-KAGERA

Leo baada ya kumtembelea moja kati ya wachongaji vinyago na mihuri aliye katika Maspaa ya Bukoba Mjini Bwn.Shafi Mustapha ameweza kutueleza mengi kuhusu shughuli zake za uchongaji na kwa namna anavyoziendesha na changamoto anazo kabiliana nazo.Akiongea na Gazeti la Hamasa Bwn.Shafi Mustapha alielezea kuwa shuguli yake kubwa anayo jishughulisha nayo katika ofisi yake ni uchongaji wa mihuli mbalimbali kama ya Mashuleni,Ofisini au ya mtu binafsi.
  Alizungumzia shughuli hiyo kama shughuli yenye manufaa makubwa kwake na ndoo kitu kinachomfanya aifanye shughuli hiyo kwa kipindi cha muda mrefu mpaka sasa, kwani shughuli hiyo ya uchongaji wa mihuri ndio inayomuwezesha  Bwn.Shafi Mustaph ambaye ni Baba wa watoto sita kuweza kuimudu familiayake katika mahitaji mbalimbali, akizidi kuliambia Gazeti la Hamasa mafanikio aliyo yapata kupitia kazi yake ya uchongaji wa mihuri alisema “kazi hii imenipatia faida kiasi cha kuweza kujenga nyumba yangu mwenyewe”.Akiwa kama moja ya wanafunzi wa kaka yake ambaye pia ni mtaalamu wa kazi hiyo Bwn.Mustapha alisema kutosomea kazi hiyo ya uchongaji wa mihuri ila ni kazi ambayo alifundishwa na kaka yake kipindi cha nyuma na alijiendeleza mpaka sasa ana ofisi yake ambamo huendeshea shughuli zake za uchongaji mihuri kulingana na mahitaji ya wateja wake mbalimbali.
 Akiendelea na mazungumzo Bw.Mustaph alielezea kwa namna kazi hiyo inayoweza kumgharimu hadi mudawa masaa matatu(3)au zaidi kwa jinsi wateja wake wanavyo ipokea na kundi gani ni sehemu kubwa ya wateja wake? Alisema”Soko na wateja wangu wengi ni watu kutoka maofisi mbalimbali,mashuleni na kwa watu binafsi.Ila changamoto kubwa ni kwa namna baadhi ya wateja hao ambavyo bado hawajauthamini ukubwa na ugumu wa kazi hii hivyo hata katika maelewano hupenda kufanyiwa kazi kwa bei ya chini sana kuliko kazi yenyewe”.
 Bwn. Mustapha ambaye ni mkongwe katika sanaa hiyo ya uchongaji wa mihuri alituelezea kwa ufupi kwa namna uchongaji wa muhuri mmoja unavyofanyika, “Shuguli hizi hutegeme na mahitaji ya mteja  lakini kwa muhuri mdogo wa kawaida hatua zake ni kuchonga maneno katika mpira mdogo na maneneo hayo yawe katika mtindo wa kiarabu yaani hutoka kulia kuelekea kushoto na baadaye huja kuwekwa katika kijibao kidogo cha muhuri.Hatua hizi chache huhitaji usanifu na ufundi mkubwa kwa ajili ya kutoa muhuri ambao utamvutia mteja.”



Batiki, vazi la kitanzania lisilochuja



HAMASA-KAGERA

KITAMBAA cha batiki kimekuwepo kwa muda mrefu, na bado hakijapitwa na wakati. Wafalme huvaa batiki wakati wa karamu zao za kifahari, na pia wachuuzi sokoni huvalia batiki. Batiki ni kitambaa maridadi, chenye rangi za kuvutia, na kina unamna-namna wa michoro. Hata hivyo, batiki ni nini? Kinatengenezwaje? Kilitoka wapi? Na kinatumiwaje leo?
Batiki ni kitambaa kilichoanza kutumiwa zamani. Michoro ya batiki hutokezwa kwa kutumia mbinu ya pekee ya kuzuia rangi isishike sehemu fulani-fulani za kitambaa na sanaa hiyo imekuwa sehemu ya maisha na utamaduni wa watu nchini Indonesia. Vitambaa vya aina hiyo ni maarufu duniani kote.
Msanii hutumia kifaa kidogo cha shaba kilichojazwa nta iliyoyeyushwa ili kuchora kwa mkono michoro mbalimbali ya pekee kwenye kitambaa. Baada ya nta hiyo kukauka, kitambaa hicho hutiwa ndani ya rangi. Sehemu zilizopakwa nta huhifadhi rangi yake ya asili, kwa kuwa hazishiki rangi. Ili kutokeza unamna-namna wa mitindo, mbinu hiyo hurudiwa tena na tena kwa kutumia rangi tofauti-tofauti.

Katikati ya karne ya 19, wasanii wa Batiki walitumia stempu za shaba kutia nta. Njia hiyo ilikuwa ya haraka kuliko kutumia kifaa cha shaba na ingeweza kutumiwa kutengeneza vitambaa vinavyofanana. Katika karne ya 20, viwanda vilianza kutumia wavu fulani uliotengenezwa kwa hariri unaowekwa kwenye mashine ili kutokeza picha kwenye kitambaa. Lakini bado unaweza kununua kitambaa cha batiki kilichotengenezwa kwa mikono. Hata hivyo, vitambaa vya batiki vinavyotengenezwa viwandani ndivyo vinavyopatikana kwa wingi.
Kwa kawaida, vitambaa vya pamba na hariri hutumiwa kutengeneza batiki. Rangi zinazotumiwa hutengenezwa kutokana na majani, mbao, maganda ya mti, na vikolezo, ingawa rangi zinazotengenezwa viwandani hutumiwa pia. Kabla ya nta kuanza kutumiwa, majani yaliyopondwa, mafuta ya wanyama, na hata matope yalitumiwa kutokeza michoro. Siku hizi nta inayotumiwa hutengenezwa viwandani.

Hata hivyo, bado watu wanatumia mchanganyiko wa mafuta ya taa na nta ya nyuki. Hakuna mtu anayejua ni lini na ni wapi hasa kitambaa cha kwanza cha batiki kilipotengenezwa. Nchini China, vipande fulani vya vitambaa vya batiki vimepatikana vinavyokadiriwa kuwa ni vya kabla ya karne ya sita W.K. Bado haijajulikana wazi ni lini mbinu ya kutengeneza batiki ilianza kutumiwa nchini Indonesia, lakini kufikia karne ya 17 inaonekana kwamba wafanyabiashara walileta vitambaa vya batiki nchini Indonesia na wengine walivinunua kutoka nchini humo.
Katika miaka ya hivi karibuni, vazi la batiki limekuwa maarufu zaidi na limekuja kuwa vazi linalotambulisha taifa la Indonesia. Mnamo 2009, ili kutambua historia ndefu ya batiki nchini Indonesia na jinsi ambavyo limeathiri utamaduni wa nchi hiyo, shirika la UNESCO liliorodhesha sanaa ya batiki kuwa sehemu ya “Utamaduni wa Kiasili Uliorithiwa” wa nchi hiyo.
Kuna njia za kitamaduni za kuvaa, kukunja, nakutengeneza batiki ambazo zinatokana na mila na ushirikina wa watu wa Indonesia. Mikoa mingi ya Indonesia ina aina zao za rangi za batiki na michoro. Kwa mfano, batiki kutoka pwani ya kaskazini ya Java, huwa na rangi nyangavu na mara nyingi zinakuwa na michoro ya maua, ndege, na wanyama wengine. Hata hivyo, batiki inayotoka Java ya kati kwa kawaida huwa na rangi chache ambazo zinakaribia kufanana, na mara nyingi zinachorwa maumbo ya kijiometriki. Kuna aina 3,000 hivi za mchoro ya batiki zilizorekodiwa.

Vazi la kitamaduni la batiki ni selendang, ambalo hutumiwa kama mtandio au nguo ya kubebea vitu ambayo wanawake huvaa au kujitanda mabegani. Mara nyingi, wanawake huitumia kama mbeleko ya kubebea watoto au bidhaa za sokoni. Hata hivyo, kunapokuwa na jua kali mtandio huo hutumiwa kufunika kichwa. Wanaume hutumia kitambaa fulani cha kitamaduni kufunika kichwa kinachoitwa iket kepala. Kitambaa hicho cha batiki chenye
umbo la mraba hufungwa kichwani na kufanyiza kilemba. Mara nyingi, kilemba hicho huonwa kuwa vazi rasmi la sherehe.Kitambaa kingine cha batiki chenye umbo la mstatili kinachopendwa sana na ambacho hufungwa kuzunguka mwili kinaitwa sarong. Wakati mwingine pindo mbili za mwisho huunganishwa. Sarong ya kawaida hufunika miguu, kisha mkunjo hufanyizwa kiunoni, na hivyo huwa kama sketi kubwa. Sarong huvaliwa na wanaume na wanawake. Vitambaa vya batiki hutumiwa kutengezaaina nyingi sana za nguo, iwe ni suruali za kawaida tu au hata magauni ya hali ya juu. Lakini vitambaa hivyo hutumika kuchorea picha, mapambo ya kuning’inizwa, vitambaa vya meza, mashuka ya kupamba vitanda, na kadhalika. Watalii wanapotembelea soko la vitambaa vya batiki nchini Indonesia wanaweza kupata aina tofauti-tofauti za mifuko, sapatu, chengeu, na hata mfuko wa kufunika kompyuta zinazoweza kubebwa. Kwa kweli, kina matumizi mengi yasiyoweza kuhesabika—kitambaa maridadi sana.



Mdau: Maendeleo hayaletwi na Makongamano bali Utekelezaji wa Mipango


Mkoa wa Kagera ni mojawapo ya mikoa kongwe kabisa hapa Tanzania. Hapo mwanzo ulijulikana kwa jina la Mkoa wa Ziwa Magharibi kumaanisha ni mkoa ulio karibu na Ziwa Victoria. Mkoa huu umejaaliwa kila aina ya neema na rasilimali. Kilimo cha ndizi na kahawa ndiyo mazao makuu kwa ajili ya uchumi wa wanaKagera. Kwa upande mwingine mkoa huu umejaaliwa shughuli za uvuvi unaoendelea katika ziwa victoria ambapo  kuna uvuvi mkubwa samaki aina ya sangara, sato na dagaa. Mbali na rasilimali zote hizi kuna watu mashuhuri ambao wametokea katika mkoa huu ambao wamechangia Maendeleo makubwa katika mikoa mingine. Lakini kumetokea changamoto kubwa ya kimaendeleo kiasi kwamba mkoa huu umetajwa kati ya mikoa maskini zaidi hapa Tanzania. Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Philip Mpango alitoa takwimu hizi wakati akiwasilisha taarifa ya tathimini  ya mwaka 2015/2016 alionesha kuwa mkoa huu una umaskini wa asilimia 39.3 wilaya ya Biharamulo inaongoza kwa umaskini zaidi. Takwimu zinaonesha kuwa wakazi wa mkoa huu wana kipato cha chini kabisa na shughuli za uzalishaji haziwaingizii kipato kama inavyostahili kulinganisha na mikoa mingine. Takwimu ya wizara ya fedha inaonesha kuwa asilimia kubwa ya wakaazi wa mkoa huu mbali na kipato cha kila mtanzania kimepanda kutoka shilingi 770,464 mwaka 2010 hadi  shilingi 1,919,928 kwa mwakabado kipato hiki hakijafikiwa na watanzania wengi wa mkoa huu. Hatuwezi kuzibeza wala kuzidharau takwimu hizi kwani zina maana kubwa kwa maisha ya kila siku ya wanaKagera. Na katika kujadili umaskini ni lazima kuweka mapendekezo ya nini kifanyike ili kukinusuru kizazi cha mkoa huu ambao una historia kubwa kwa Maendeleo ya taifa hili.
Kilimo na ufugaji, huu ni utimgongo wa watanzania wengi lakini katika mkoa huu wakulima wengi hawalimi kwa ajili ya biashara bali hulima kwa ajili ya kula tu (subsistence) ambapo inakuwa ngumu kwao kushindana na uzalishaji wa mikoa mingine. Kilimo cha mkoa huu kimekuwa cha mazoea sana kiasi kwamba wakulima hawajibadilisha fikra zao na namna ya uendeshwaji wa kilimo. Zao la ndizi ambalo limetegemewa kwa karne nyingi limekumbana na ugonjwa wa mnyauko(Banana Xanthomonas wilt) ambapo uzalishaji wa ndizi umepungua kwa kasi sana. Kilimo kinapaswa kubadilishwa kwa wakulima kulima mazao mbadala kama viazi, ufuta,mihogo na mazao ambayo sio ya msimu. Aidha kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kwa wananchi kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji. Mkoa huu umejaaliwa mito na mabwawa pamoja na maziwa kadhaa ambayo yanaweza kuwa chanzo cha maji. Mwambao wa Mto Ngono ni mojawapo ya eneo lenye rutuba kubwa kinacho hitajika ni kuweka utaratibu wa vikundi kwenda kuanzisha kilimo cha mazao ambayoyanaweza kuwa ya chakula na biashara pia. Kilimo cha umwagiliaji kinaweza kutatua tatizo la chakula hapa mkoani. Biashara, sekta ya biashara ni moja wapo ya sekta ambayo ina manufaa makubwa sana mkoa huu una bahati ya kuwa mpakani na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda ambazo zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha mahusiano ya kibiashara kwa wakazi wa mkoa huu. Mipaka inapaswa kutumika kama kitovu cha uchumi wa mkoa huu, kuna bidhaa ambazo hazipatikani katika mataifa jirani ambazo wananchi wakihamasishwa wakasafirisha mpaka huko wanaweza kupata masoko pamoja na mahusioano mema ya kibiashara. Lakini pia biashara ya ndani kwa ndani ni mojawapo ya kitu muhimu kwa wananchi pamoja na uchumi wa mkoa mzima. Biashara zote kubwa na ndogo zinapaswa kuwekewa utaratibu mzuri ambao utawanufaisha wafanyabiashara na wananchi. Pia uwekezaji kwenye bidhaa za chakula nafaka pamoja na biashara ambazo zinaendana na kasi ya karne hii. Wadau wa Maendeleo, mkoa huu una watu mbali mbali ambao wameendelea kiuchumi lakini hawajaweza kujiwekeza katika mkoa huu ili  kuwanufaisha wakaazi wa mkoa huu.Aidha juhudi za wadau hawa kamwe hazitoshi, kumekuwa na makongamano pamoja na vikao vya wadau wa Maendeleo wa mkoa huu ambavyo havijazaa matunda kwani ushirikiano unakuwa ni mdogo au ushirikiano na walengwa unakuwa ni mdogo sana. Kwa upande mwingine Maendeleohayawezi kuletwa na watu waliopo mbali ila ni juhudi za watu waliomo ndani ya mkoa kwani waliopo nje huweza kuja wakiona kuwa waliopo ndani wametia nia na juhudi za kujikwamua kimaendeleo.
Uvuvi, sekta ya uvuvi ni mojawapo ya maeneo ambayo yanaweza kulikuza pato la mkoa huu. Kuna maziwa kama Ikimba,Burigi, Victoria pamoja na mito mikubwa ambayo ipo mkoani kama Kagera na Mto Ngono. Lakini kwa takwimu zilizopo ni kwamba samaki wengi wanaotumiwa Rwanda wanasafirishwa kutoka Mwanza jambo ambalo linapaswa kubaki aibu kwa wafanyabiashara na wavuvi wa mkoa wa Kagera. Sio kwamba samaki hawapo ila tatizo ni mfumo wa uvuvi pamoja na mawazo ya wavuvi. Mfano takwimu zinaonesha kuwa kipato cha uvuvi kimeshuka kutoka tani kilo 150 kwa mtumbwi hadi kilo 15 kwa mtumbwi. Njia za uvuvi zinazotumika bado ni za kiasili na wavuvi wengi wamelenga soko la ndani tu. Kilimo cha uvuvi kinapaswa kuimarishwa sana kwa kuhamasisha uvuvi wa kisasa na kuweka misingi ambayo mazao ya uvuvi yatapata soko la ndani na nje.

Kwa upande mwingine mkoa huu una vivutio kadhaa vya utalii ambavyo vikitangazwa  vyema vitakuwa chachu ya kuwaleta watalii na kuinua biashara za mahoteli pamoja na kuutangaza utamaduni wa mkoa wa Kagera. Utamaduni wa ngoma, mavazi chakula vikitumiwa kisawa sawa ni jambo muhimusana katika kuukuza utalii na mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi. Maendeleo ni mojawapo ya kilio cha watanzania wengi, kuna umuhimu mkubwa wa wakazi wa mkoa huu waliopo ndani na nje kuweka na kutekeleza mipango mikubwa kwa ajili ya kuinua kipato chao. Juhudi za serikali pekee hazitoshi kuinua kipato na kuondoa umaskini. Mikoa mingi ambayo imeendelea haijaendelea kwa sababu ya juhudi za serikali ila ni juhudi za wananchi pekee na serikali inakuwa chanzo cha kuweka utaratibu ili mwananchi wanufaike.
 Pia nguvu kazi ambayo ni vijana inapaswa itumike kisawa sawa kwani inaonekana kuwa vijana wengi siku hizi wanakimbilia mijini na kufanya kazi ambazo zinaingiza kipato kwa muda mfupi. Hii hurudisha nyuma uzalishaji wa mazao na chakula. Vijana kama nguvu kazi inapaswa wawe watu wa kwanza kabisa katika mchakato wa kuleta Maendeleo kwa jamii. Vijana wakiwa katika vikundi au mmoja mmoja wawekewe utaratibu mzuri ambao watatumia fursa zilizopo kwa kila mkoa kwa manufaa ya vizazi vijavyo pamoja na kizazi hiki. Pia Maendeleo hayawezi kuletwa kwa vikao na makongamano bali kuna umuhim mkubwa wa kutekelea miradi na mipango ya Maendeleo kwa ajili ya manufaa ya wanaKagera.

Maoni ya WEKISHA K KARUMNA (Mwanafunzi wa UDSM na Mkazi wa Muleba)

HISTORIA YA MWANAMASUMBWI HAYATI MUHAMMAD ALI

NA DIDAS MUGYABUSO
(Kwa msaada wa Mtandao)


Hayati Muhammad Ali anayeaminika kuwa moja ya wanamasumbwi bora wa mda wote duniani alikuwa bondia kwa sababu kuna mtu aliyemuibia baskeli yake. Alikuwa na umri wa miaka 12 wakati ule na ali¬kuwa akiishi Louisville katika jimbo la Kentucky akijuilikana kwa jina la Cassius Mercellus Clay Jr.
Siku ya tukio hilo alikuwa na rafiki zake wakitafuta peremende na porp corns za bure.
Alipogundua kwamba baiskeli yake imeibiwa  aliagizwa kwende chini ya nyumba aliyokuwepo katika taasisi ya mafunzo ya Columbia ambapo afisa wa polisi Joe Martin alikuwa akisimamia mpango wa ndondi.Martin alimwelezea Ali kwamba aanze kunoa ngumi zake kwa kujifunza ndondi kabla ya kumtafuta mwizi huyo. Joe Martin, aliyekuja kuwa kocha wake baadaye, anaelezea jinsi kijana huyo alivyokuwa akilia huku akiahidi kumtandika ngumi aliyemuibia baiskeli yake pindi akimpata. Kocha huyo wa ubondia aliyekuwa Polisi wakati huo alimchukua Clay, kijana mweusi anayetokea katika familia ya watu maskini, na kumjumuisha na watoto wengine aliokuwa akiwafundisha.“Alikuwa na bidii zaidi kuliko waatoto wote wengine niliokuwa nikiwasimamia,” anasema Joe Martin.
Ingawa Clay wakati ule hakuwa na nguvu ya kuvurumisha masumbwi, alikuwa mwepesi wa kuranda randa kupita kiasi. Mnamo mwaka 1960, akiwa na umri wa miaka 18, alishinda katika pambano la ndondi la michezo ya Olympiki mjini Rome, Italia. Medali yake ya dhahabu inasemekana aliitupa ndani ya Mto Ohio kwa sababu alikasirishwa na jinsi watu weusi wanavyobaguliwa nchini mwake. Cassius Clay alikamilisha michuano ya wasiolipwa baada ya kuibuka na ushindi mara 100 katika jumla ya mapambano 108 aliyopigana. Wafanyabiashara 11 wa Kizungu kutoka Louisville walishirikiana ili kumfungulia njia Cassius Clay ya kuingia katika ulingo ya mabondia wa kulipwa.Bondia huyo mwenye kipaji alikuwa akijulikana pia kuwa ni mtu aliyekuwa na majivuno na mdomo mpana. Kabla ya mapambano yake, Cassius Clay daima alikuwa akijitapa kuwa yeye ndie mbabe wa wababe na mzuri

kuliko mabondia wote na kuwakejeli wapinzani wake. Mtindo ambao umekuwa ukitumiwa pia na mabondia wa kileo kama Floyd Mayweather, na hapa Tanzania umekuwa ukitumiwa na mabondia kama Mada Maugo na Francis Cheka. Katika pambano lake la kwanza la kuwania ubingwa wa dunia Februari 1964 dhidi ya mtetezi wa taji hilo, Sonny Liston, Clay hakuwa akijulikana ni nani na watu waliamini angeshindwa tu. Lakini baada ya raundi ya sita, Liston aliungama. “Mie ndie mbabe,” alinguruma Cassius Clay kupitia kipaza sauti.
Mwaka huo huo, alisilimu na kujiunga na kundi la Nation of Islam lililokuwa likiongozwa wakati huo na mwanaharakati wa haki wa Wamarekani Weusi, Malcolm X. Akabadilisha jina la Cassius Clay na kujiita wakati huo huo Muhammad Ali.Muhammad Ali hakuwa bondia tu, alikuwa mwanaharakati pia. Alipinga vita vya Marekani nchini Vietnam na alikataa kutekeleza sheria ya kutumikia jeshi. Mnamo mwaka 1967, akapokonywa sio tu leseni yake ya ubondia, bali pia alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela, ingawa baadaye bondia huyo wa aina pekee aliachiwa kwa dhamana.Wasanii na wasomi mfano wa Richard Burton na Henry Fonda au mwandishi vitabu Truman Capote wakampigania mpaka Muhammad Ali akaruhusiwa tena kurejea ulingoni baada ya kulazimika kukaa nje kwa miaka mitatu. Machi 8, 1971 Muhammad

Ali aliteremka ulingoni Madison Square Garden mjini New York kwa kile kilichotaajwa “kuwa pambano la ndondi la karne” dhidi ya bingwa wa wakati ule, Joe Frazier. Lilikuwa pambano kati ya mafahali wawili, kati ya mpinzani na yule aliyekuwa akiangaliwa kama mwakilishi wa mtindo wa maisha wa Kimarekani. Katika pambano hilo la kusisimua la zaidi ya raundi 15, Frazier akashinda kwa pointi. Ali akalazimika kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya ubondia kunusa jamvi.
Yakafuata mapambano mengine ya kusisimua mfano wa lile la mjini Kinshasa dhidi ya George Foreman mnamo mwaka 1974, ambapo Muhammad Ali anasema aliranda mfano wa kipepeo na kuuma kama nyuki ‘Float like butterfly, sting like a bee’
Muhammad Ali alilipiza kisasi dhidi ya Joe Frazier mwaka 1975 na kumlazimisha kusalimu amri mnamo rauni ya 14. Mohammed Ali alistaafu mwishoni mwa mwaka 1981 baada ya kukaa ulingoni kwa zaidi ya miaka 25 .
Wakati huo tayari alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya Parkinson. Licha ya maradhi hayo, Muhammad Ali ndiye aliyewasha mwenge wa Olimpiki huko Atlanta mnamo mwaka 1996 na kuusisimua ulimwengu mzima. Mwaka 1999 aliteuliwa na kamati kuu ya michezo ya Olimpiki kuwa “mwanaspoti bora wa karne.”
Mpinzani wake wa zamani George Foreman amegeuka hivi sasa kuwa rafiki yake

mkubwa na kuungama “Muhammad Ali ndie bingwa wa mabingwa.” Mpaka June 4 2016 Muhhamad Ali anapoteza maisha ndie mwanamasumbwi mstaafu kutoka nchini Marekani. aliepata kuwa bingwa wa uzito wa juu mara tatu.

Je, mastaa wanasemaje kuhusu Muhammad Ali?
Haya ni maneno ya Rais wa zamani wa Marekani kipindi Ali anatimiza miaka 70 ya kuzaliwa;“Ustadi, haiba na misimamo isiyoyumba ya Muhammad Ali ndio mambo yaliyosaidia kuufanya mchezo wa masumbwi kuwa maarufu duniani”“Watu waliacha kuupenda mchezo wa ngumi. Katika miaka ya 1940 na 1950 ulikuwa ni mchezo maarufu sana Marekani na baadae umaarufu huo ukapotea,” aliimwambia mtangazaji wa masumbwi wa BBC Mike Costello.
“Baadae akachomoza Muhammad Ali, awali akiitwa Cassius Clay, akionekana sawa na mcheza dansi katika ulingo wa masumbwi - akiwakumbusha watu huo ulikuwa ni mchezo.
“Aliurejeshea mchezo huo msisimko na kuwa wa maana tena. Alikuwa akiburudisha na alipokuwa kijana alikuwa akizungumza sana. Lakini ilikuwa ni sehemu ya madoido yake.Joe Bugner (Mwanamasumbwi aaliyewahi kupigwa na Ali mara 2)
“Alikuwa ni mwanamichezo zaidi ya mwanamasumbwi. Alikuwa ni mwanamichezo
Frank Bruno
“hatutaweza kumshuhudia bondia mwengine kama alivyokuwa Ali, aliiuweka mchezo wa masumbwi katika ramani”.
“Alifungua njia kwa wanamasumbwi kama mimi kupenda mchezo huo na kujipatia kipato,” alisema Bruno.
George Foreman: Mwanamasumbwi aliyewahi kupambana na Mohammed Ali katika mechi iliyofanyika Zaire (Sasa DRC) kabla ya Ali kuibuka mshindi, anasema kuwa Mohammed Ali alikuwa na ushawishi wa kukufanya umpende. Iwapo usingempenda angekufanyia vituko zaidi ili uweze kumchukia zaidi.
Florah Mosha: Moyo wangu unanung’unika kwa kumpoteza mwanzilishi, bondia hodari, bingwa na shujaa kwa vyovyote vile. Hakuna siku niliingia katka ulingo wa ndondi bila kumkumbuka , alisema katika mtandao wa instagram. Ucheshi, uzuri wako na vinginevyo ndio vitu tutakavyovienzi.Julia Hassan: Kila mara nilihisi Mungu alimfanya Muhammad kuwa mtu muhimu, lakini sijui kwa nini Mungu alinichagua mie kumbeba mwana huyu, wakati alipokuwa mtoto hakuweza kutulia, alitembea na kuzungumza na kufanya kila kitu wakati wake. Akili yake ilikuwa kama upepo unaovuma na kueleka kila sehemu.Rahman Ali: Nduguye Mohammed Ali anasema kuwa marehemu alikuwa akimtaka amrushie mawe, nilidhani ameshikwa na wazimu, lakini mawe hayo angeyakwepa yasimpige kumpiga.John Alex: Ndio mwanamichezo hodari mweusi niliyewahi kumjua na ana umuhimu mkubwa kwa watu wake. Kwa sababu mabilioni ya watu kutoka Afrika, Asia na Arabia wanakupenda lazima ujue majukumu yako.
Jesse Jackson:Walikataa kusikiliza ushuhuda wake kuhusu dini yake. Walijaribu kumnyanyasa, walijaribu kumuathiri kimwili na kiakili.
Bingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa uzito wa juu duniani, Mohammad Ali aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana, aliwahi kuzuru nchini Tanzania mwaka 1980.

Wamachinga Manispaa ya Bukoba bado hali tete..

  NA YEGESA MABALA-BUKOBA

Wafanyabiashara ndogondogo  almaarufu kama wamachinga katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wameiomba Serikali  kupitia  Manispaa ya Bukoba  kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika eneo jipya la machinjio ya zamani ambapo wamehamishiwa kutoka katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maeneo ya Shaburidini,  maeneo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera(Government) maarufu kama Uganda Road  pamoja  na maeneo tofautitofauti  ya Manispaa hiyo ya Bukoba Mkoani Kagera.
Kauli hiyo ilitolewa na baadhi ya wafanyabiashara hizo ambapo ni pamoja na Bi: HUSNA MOHAMED,Respikius Salatieli na mwingine aliye tambulika kwa majina ya Hashimu Mohamedi wote wakiwa wafanyabiashara wa soko hilo jipya la machinjioni barabara ya Kashozi iendayo Migera Katika Manispaa hiyo ya Bukoba .
Wafanyabiashara  hao wamesema kuwa changamoto kubwa ambayo inawakabili kwa sasa ni pamoja na kutokuwepo kwa ulinzi wa kutosha katika soko hilo ambapo mali zao walisema kuwa haziko katika usalama, muda wote wanawaza pa kuzipeleka wapi pindi wanapofunga na kuondoka kwenda majumbanikwao ambapo wamesema  kuwa ulinzi katika eneo lao hilo unahitajika ili wawe wanaacha biashara zao na kurejea majumbani kwao pasipo kuwa na mashaka yoyote juu ya biashara zao hizo .
Walisema pia Halmashauri ya manispaa hiyo inatakiwa kuwasimamia katika kufanya biashara hiyo kutokana na baadhi ya wamachinga hao kuwa katika vikundi viwili ambavyo ni pamoja na kikundi cha kwanza kushindwa kupanga bidhaa zao ndani ya soko hilo ambapo walipewa eneo na kujenga vibanda lakini cha kushangaza baadhi ya wamachinga wenzao wanashindwa kupanga biashara zao na kuamua kupanga bidhaa hizo mbele kwa kutandaza chini hali ambayo pia wanalalamikiana wao wenyewe katika kile ambacho walisema wanazibiana riziki kw akuwa wateja walio wengi ni wapiti njia na hivyo wanakomea mbele kwa walio tandaza chini na waliomo ndani kushindwa kufikiwa na wateja hao. Hata hivyo Machinga hao walizidi kusisitizakwa kuiomba Serikali kuhakikisha inawaondoa pia wafanyabiashara hao ndogondogo ambao wapo katika maeneo ya stendi Kuu ya mabasi kwa kuwa wameanza kurejea katika maeneo hayo ambayo waliamuliwa kuondoka  kwani kuna huduma zingine ambazo zinahitajika katika soko hilo ambapo zinakosekana kutoka na baadhi ya machinga hao kuwa katika eneo hilo la stendi ya mabasi na hivyo kufanya wanunuzi kutoka eneo hilo na kwenda kutafuta eneo jingine na hivyo kuiomba Serikali kulishughulikia suala hilo.
Kadhalika walisema kuwa eneo hilo ambalo wanafanyia biashara hiyo hawana  uongozi ambao pengine wangeweza kuwasilisha kero zao na walisema kuwa inakuwa vigumu sana katika kwenda kwa pamoja kuwasilisha matatizo yao katika uongozi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo jambo ambalo pia bado ni changamoto katika kupata hatima ya biashara zao. Hata hivyo Gazeti hili la HAMASA lilifika katika viwanjavya machinga hao mnamo mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Diwani wa kata ya Kahororo ambae pia ni Meya wa Manispaa ya Bukoba Mhe: Chief Kalumuna aliwaambia wamachinga hao kuwa matatizo yao hayo yote ambayo yanawakabili yapo mbioni kutatuliwa  na kuwataka machinga hao kuwa wavumilivu pia Serikali ya Mkoa huo wa Kagera kupitia Manispaa hiyo inatambua umuhimu wa wafanyabiashara hao .
Vilevile alipokuwa akiongea nao wamachinga waliweza kumtambulisha uongozi wao mpya walioamua kuuchagua baada ya kuona barua yao ya kuomba uongozi kuchelewa kujibiwa. HAMASA ilifanya mahojiano mafupi na Mwenyekiti aliyechaguliwa na kusema, “Tuliandika barua ya maombi kuhusu uongozi wa soko la machinjioni kwa mtendaji kata Kashai wakaomba tusubiri, baada ya kuchelewa na changamoto kuwa nyingi tukakubaliana kuchagua uongozi wa muda siku ya taehe 25 mwezi huu ambapo mwenyekiti ni mimi Leonidas Kalyamtima, katibu ni Jovonati Clemence na muweka hadhina ni Husna Mohamed” Alimaliza.
Kwa upande wa Meya aliwaambia wamachinga kama wataridhia hao ndo wawe viongozi wao basi wao hawana tatizo, uongozi huo utathibitishwa siku ya kikao rasmi ambacho bado hakijafanyika.










UWANJA WA KAITABA NI KWA AJILI YA LIGI KUU TU

BUKOBA MICHEZO                          

Siku chache baada ya uwanja wa kaitaba kukamilika,wananchi mkoani Kagera wameshauriwa kuacha mazoea ya kutumia uwanja huo kama ilivyokuwa zamani ikiwa ni pamoja na kuwekwa utaratibu na ratibainayoeleweka kwa matumizi ya uwanja huo. Akiongea na gazeti hili afisa michezo wa mkoa  kagera bw. Kepha Elius alisema kuwa kwa ushauri waliopewa na kandarasi wa uwanja huo,alisema ni vyema utumike kwa michezomichache ili uweze kupata muda wa kupumzishwa kwani unaweza kudumu kuanzia miaka 8-15 bila kuharibika,huku akishauri kuwa ni bora uwanja huo utumike kwa michezo ya ligi kuu na kwa ligi za kawaida uwepo utaratibu wa kutumia viwanja vingine lakini hata ikiwa kaitaba isiwe kila mara.

Kwa upande mwingine Bw.Kepha alilipongeza shirika la Jambo Bukoba kwa mpango wao mzuri wanaoendelea nao wa kuboresha uwanja wa Nshamba Tapa uliopo wilayani Muleba na uwanja wa Kihanga uliopo wilayani Karagwe,maana hali hiyo itaupunguzia mzigo uwanja wa Kaitaba ikiwa ni pamoja na kuendelea kukuza vipaji vya michezo mkoani Kagera.
Kufuatia hali hiyo amezishauri halmashauri zote mkoani Kagera kuendelea kuboresha viwanja vya michezo katika maeneo yao na kusimamia michezo ya aina zote,na kuongeza kuwa halmashauri ya manispaa ya Bukoba inatakiwa kukamilisha maboresho ya maeneo mengine  katika uwanja wa kaitaba na aliwapongeza kwa hatua nzuri waliofikia tangu walipokabidhiwa uwanja huo na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania(TFF).
Akiongelea muamko wa michezo mkoani Kagera alisema kuwa bado wanakabiliwa na changamoto ya wadhamini,na wakipatikana wanajikita zaidi kwa mchezo mmoja wa mpira wa miguu hali inayoendelea kudidimiza  michezo mingine mkoani  humo,na aliwaomba wafadhili kubadilika na kuwa na muamko kwa michezo yote ili  kuwasaidia wanakagera wenye vipaji katika Michezo hiyo.
Katika hatua nyingine bw.Kepha alisema kuwa  mkoa wa Kagera upo kwenye mpango wa kuanzisha mchezo wa mbio za polepole(Jogging club)ambao utasaidia kuimarisha afya kwa watakaopenda kushiriki,na aliongeza kuwa kupitia hapo wataweza kufanya hata mazoezi mbalimbali ya viungo vya mwili ambayo yatakuwa yanafanyika katika wiki ya usafi ya mwisho wa mwezi  kuanzia saa kumi na mbili za asubuhi  kwa kuzunguka maeneo mbalimbali katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Uwanja wa Kaitaba uliopo Manispaa ya Bukoba kama unavyoonekana kwa sasa

FIESTA MULEBA


Lile tamasha kubwa la Muziki Tanzania, FIESTA linaloandaliwa na Clouds Entertainment siku ya tar 28 Agosti lilitua mjini Muleba kwenye kiwanja cha Zimbihile ambapo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kukata kiu ya mashabiki wa muziki wa kizazi kipya ‘BongoFleva’ wa maeneo hayo na maeneo ya jirani kwa kushuhudia wasanii wengi wakubwa wakitumbuiza laivu, lakini pia kupitia jukwaa la Fiesta tuliweza kuvitambua vipaji vipya vya nyumbani, kwani kulikuwa na msululu wa zaidi ya wasanii 30 waliopewa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao kutoka mkoani Kagera.

Orodha ya wasanii wa Dar es salaam waliotumbuiza ni; Shilole, Mr Blue, Maua Sama, Bilnas, Jux, Raymond, Nandy, Baraka Da Prince, Darasa, Stamina, Navy Kenzo, Chege, Christian Bella, Msami, ManFongo, Shollo Mwamba, Edo Boy na Bonge La Nyau.

Wasanii waliofanikiwa kupata shangwe nyingi ni Joh Makini, Stamina, Mr. Blue, Chege, Baraka De Prince na Jux huku katika hali isiyotarajiwa yule mkali wa kisingeli Man Fongo ‘Nshomile’ wakashindwa kumuelewa kabisa na kubaki wakimuangalia tu mda mwingi alipokuwa jukwaani bila kumpa ushirikiano wowote.

Pia kwa upande wa wasanii wa nyumbani ni wengi sana waliopata nafasi ya kupanda jukwaani, wasanii zaidi ya 30 walipata nafasi hiyo huku msanii aliyetambulika kwa jina la Love B akionekana kufunika zaidi na michano yake (Rap) sambamba na msanii Obed Moses ‘O-Strings’ aliyefanikiwa kuibuka mshindi wa shindano la super nyota, na kupata nafasi ya kwenda Dar es salaam kwa ajili ya fainali za shindano hilo. Msanii mwingine wa nyumbani aliyeonekana kukubalika ni Mr. Mos aliyepigiwa shangwe baada ya kuimba wimbo wake wa ‘Kazi ya kidole’.

Gazeti la HAMASA lilijaribu kupiga stori na wadau wawili waliohudhuria Tamasha la FIESTA la mwakajuzi Kaitaba mjini Bukoba na hili la Muleba kiwanja cha Zimbihile na kusema hili la mwaka huu ni ‘funiko’, watu walikuwa wengi zaidi na wasanii waliotumbiza walijipanga sana.
Hili limekuwa kinyume na matarajio ya wengi, wakidhani Tamasha lingekosa mvuto kutokana na kushindwa kufanyika Bukoba mjini .













Kufungwa kwa KAT Wazee wa Torrent Kuisoma Namba

NA DIDAS MUGYABUSO

Kwa wenzangu wataalamu wa masuala ya ICT hili habari sio ngeni kwao, ule uwanja wetu pendwa wa kupakua kilakitu bure ‘KickAss Torrent (KAT)’  haupo tena nasi, tovuti hii iliyojizolea umaarufu kwa takribani miaka 8, ilituwezesha kushusha ‘ku-download’ Programu mbalimbali, Muvi, Vitabu,Games, Miziki, n.k, hii ilitokea mnamo tarehe 20 Julai mwakahuu, na ilikuwa ni pigo kubwa sana kwa walevi wa mtandao huu. Ni pigo kwakuwa ni watu wengi sana walikuwa wakiutegemea huu uwanja kuendesha shughuli zao, kwa mfano kwa hapa Tanzania ni watumiaji wachache wa kompyuta ambao wamekuwa na spirit ya kutoa dola 20 hadi 100 kwa ajili ya kununua Antivirus, ama dola 100 hadi 300 kwa ajili ya kununua Window na programu nyingine za Kompyuta. Hata ukienda kwa mafundi wa Kompyuta programu nyingi wanazotumia kwa wateja sio ‘Genuine’, nyingi ndo hizi tunazozitoa kwenye tovuti za wizi kama hii KAT, kwa  ‘maana hiyo ni wengi tutaisoma namba’ kwenye hili.
Nani kaufunga? Mtandao huu umefungwa na Marekani kwa kosa la kusambaza ‘contents’zenye thamani ya zaidi ya $1 bilioni kinyume na sheria.Lakini huu sio mtandao wa kwanza kufungwa na Marekani, mitandao kadhaa kama The Piratebay uliwahi kufungwa miaka michache iliyopita
Nani Mmiliki wa KAT? Ni Artem Vaulin kijana wa miaka 30, raia wa Ukraine, alikamatwa akiwa nchini Poland. Kijana huyu alitengeneza dola milioni 12 kwa mwaka kutokana Na matangazo kupitia KAT.
kampuni ya Facebook na Apple Inc washiriki katika kukamatwa kwa Vaulin Mchakato ulianzia kwa IRS agent kuomba kuweka matangazo kwenye tovuti ya KAT, makubaliano yaliyofanyika baina ya mmiliki wa KAT na mwakilishi rasmi wa kampuni ya IRS agent. Tangazo lilipoanza kwenda hewani, iliwapa nafasi IRS ku’track’taarifa za kutosha kuweza kuhusisha KAT  na akaunti ya benki ya Latvian. akaunti ambayo baadaye iligundulika wamepokea takriban dola milioni 31 katika amana kati ya Agosti mwaka 2015 na Machi 2016.

Baada ya uchunguzi mkali wa hapa na pale, timu hiyo ya wakaguzi iliweza kutambua email ambayo alikuwa si tu na uhusiano na tovuti, lakini pia katika channel rasmi za tovuti katika mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na Facebook.

Hatua iliyofuata Apple walijaribu kukamilisha mchezo kwa kutoa taarifa ambayo inawezekana ndiyo ilikaba shughuli zote za akaunti ya Apple iliyokuwa ikimilikiwa na Vaulin.

“Records provided by Apple showed that tirm@me.com conducted an iTunes transaction using IP Address 109.86.226.203 on or about July 31, 2015. The same IP Address was used on the same day to login into the KAT Facebook Account. Then, on or about December 9, 2015, tirm@me.com used IP Address 78.108.181.81 to conduct another iTunes transaction. The same IP Address was logged as accessing the KAT Facebook Account on or about December 4, 2015.”
Apple walitoa taarifa Julai31, 2015 kuonyesha kwamba ku email hiyo ilitumika nunulia kitu kwenye iTunes na kisha IP address hiyohiyo ikatumiwa kupata access kwenye ukurasa wa Facebook wa KAT.
Kwa ufupi hivyo ndivyo muvi ya KAT ilipoishia. Je, kutapatikana mbadala wake ama ndio tutaendelea kuisoma namba?



UTALII WA UTAMADUNI MKOANI KAGERA

Hivi vitu pichani ni baadhi ni vya kiutamaduni wa Mhaya ambapo vinapatikana Makumbusho ya Kagera (Kagera Museum)
NA FRANK JOHNSON
Kwa Tanzania,kabila la wamasai ndio pekee linalonufaika na Utalii wa utamaduni, ni utalii ambao mtu anaenda sehemu moja kwenda nyingine kujifunza au kuona mambo ya kitamaduni ya jamii husika kama maisha ya watu,ngoma,chakula,mila na desturi,mtalii anaweza kwenda kuona jamii husika kwenye makazi yao au kwenda kwenye nyumba au sehemu zilizohifadhiwa vitu mbalimbali vya kumbukumbu vilivyotumiwa na jamii husika au ambavyo vinaendelea kutumiwa sasa mfano vikapu,mkuki nakadhalika. Kwa nchi zinazoendelea huu utalii umekuwa mpya kwao lakini utalii unatumiwa na nchi zilizoendelea kama Ujerumani,Uingereza na Marekani na unaingizia serikali mapato makubwa.Mkoa uliopakana na nchi nyingi zaidi Tanzania (Mkoa wa Kagera) umejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo pia utamaduni ambao tukifanikiwa na kuutangaza tutapata wageni wengi sana kuja kuona utamaduni na utaingizia jamii mapato na kupunguza umaskini. Wamasai kutokana na kufanikiwa kuutangaza utamaduni wao,wageni wengi wanaokuja kutembea Tanzania uenda kujifunza na kuwatembeleana kununua vitu mbalimbali vinavyotengenezwa na wamasai. Familia za kimasai zinanufaika sana na utalii wa kiutamaduni na wanaingiza pesa nyingi sana ,wengine hufanikiwa kuingiza hadi sh. 40,000 kwa siku  kutokana na utalii huu wa kiutamaduni.
Utalii wa kiutamaduni una nafasi kubwa sana ya kutoa ajira nyingi na kuingiza kipato kwa mkoa wa Kagera na mikoa mingine ya kanda ya ziwa na kupunguza umaskini uliopo. Mikoa ya kanda ya ziwa imetajwa kwenye ripoti ya serikali kama mikoa duni zaidi japo ina fursa nyingi lakini wananchi wanashindwa kuzitumia sababu ya kukosa elimu.
Mambo ambayo mkoa wa Kagera wanaweza kufanya kutangaza utalii wa kiutamaduni kwanza kutangaza ngoma za asili za makabila mbalimbali yanayopatikana mkoani Kagera,wasanii kama Maua na Saida wamejitaidi sana kutangaza utalii wa ngoma na walifanikiwa kuteka soko la Taanzania na nje ya nchi hivyo inaonesha ni kiasi gani utalii wa kiutamaduni wa mkoa wa Kagera unavyokubalika.
Pili utamaduni wa kumenya ndizi, wageni wengi hasawazungu hawajui jinsi ya kumenya ndizi na huwa wanashangaa mtu anavyoweza kumenya ndizi kwa haraka,kama tukiweza kutangaza utamaduni huu wa kumenya ndizi,wageni wengi watakuja kujifunza kwenye familia mbalimbali namna ya kumenya ndizi na wananchi watanufaika kwa kuongeza kipato na mkoa pia utanufaika.
Tatu mkoa wa Kagera ili kukuza na kutangaza utalii wa kiutamaduni,kila wilaya au mkoa uwe unaandaa siku ya utamaduni na kualika watu mbalimbali kuja kuona utamaduni wa sehemu husika, hii itasaidia kutanga utalii wa kiutamaduni na jamiiitanufaika sana kwa mapato.Wilaya ya Karagwe wamefanikiwa kwa hili kuandaa siku ya utamaduni wa wanyambo na wamefanikiwa kutangaza utalii wao, ni vizuri jitihada zikiendelea za kutangaza utalii huu wa utamaduni.
 Nne mkoa wa Kagera ili kutangaza utalii wa utamaduni nashauri watangaze zaidi nyumba au sehemu zinazohifadhi mambo ya utamaduni, kwa muda mrefu kumekuwa nasehemu zinazotunza mambo ya kale lakini kumekuwa hakuna jitihada kubwa kutangaza hizi sehemu. Serikali ya mkoa inaweza kunufaika sana na utalii huu kama jitihada zikiwekwa za kutangaza.Mwisho ili kupunguza umasikini mkoa wa Kagera hatuna budi kutangaza utalii huu wa utamaduni,mkoa umebahatika sana kuwa na vivutio vingi vya asili na utamaduni ikiwemo pia nyumba za asili na historia ya utamaduni wa makabila mbalimbali yanayopatikana mkoa wa Kagera. Ni wakati sasa wa kutumia fursa hizi ili kunufaika nazo na kipato kwa wananchi kiweze kukua.
   



Tambua jinsi ya kujikwamua kiuchumi wewe mwanakagera kupitia kwa wadau wa elimu.

Na Lameck Richard-BUKOBA

Tambua jinsi ya kujikwamua kiuchumi wewe  mwanakagera kupitia kwa wadau wa elimu.
  Kutokana na wimbi kubwa la vijana kukumbana na changamoto ya kukosa ajira pindi wanapohitimu masomo yao katika vyuo mbalimbali mkoani Kagera na Tanzania kwa ujumla, hali inayopelekea kuwepo kwa makundi ambayo yanaweza kuhatarisha maisha ya wnanchi kwa sababu ya kukosa kazi ya kufanya.
   Gazeti hili liliongea na mdau wa elimu mkoani kagera pia mkurugenzi wa chuo cha King Rumanyika Bw.Godison Rwegasira, ambapo alisema kuwa kuna changamoto kubwa inayowakabili wahitimu wa vyuo mbalimbali huku akisema kuwa wahitimu hao wanajisahau kujihusisha hata na kazi za ujasiliamali,na pengine kwa kutopata elimu hiyo kutoka waliposomea au kutofatilia.
    Bw.Godison alisema kuwawao wameanzisha taasisi ya elimu kwa lengo la kuondoa ujinga katika taifa letu na kuwasaidia vijana kuajiriwa au kujiajiri na kuwasaidie wananchi wengine ikiwa ni pamoja  na kujikwamua kiuchumi kupitia ajira wanazozipata.
  Kupitia hilo aliwashauri wadau wengine wa elimu na wamiliki wa vyuo mkoani kagera kuhakikisha wanatoa hata elimu ya ujasiliamali kwa wanafunzi wao  kwa ajili ya kuwawekea mazingira mazuri wahitimu ili pindi wanapokuwa nyumbani wakisubiria
 kuajiriwa wawe wanaendelea na majukumu mengine.
Aliwashauri  vijana wote waliobahatika  kwenda vyuoni kuacha tabia ya kulalamika sana kuwa hawana la kufanya kutoka na ajira kuchelewa,kwani watambue kuwa kuna mambo mengi ya kufanya katika jamii kwa kutumia elimu walioipata na aliongeza kuwa hata wale ambao pengine kwa bahati mbaya hawakuweza kujiendeleza miradi. Alisema kuwa hata kilimo,taasisi binafsi kielimu wasikae ndani kwa kudai kuwa hamna kazi kwani watambue kunani sehemu moja wapo iliyowasaidia watu wengi kutoka kimaisha,hivyo vijana wasidharau kazi  na wasipendelee kuwa na mafanikio ya muda huo huo,bali wawekeze kwanza ili baadae waweze kunufaika na kile watakachokianzisha na pale watakaposhindwa wanaweza kuongea na hao wadau wa maendeleo au watu waliopiga hatua kimaisha ili kuhakikisha wanasonga mbele kimaendeleo.

   Bw.Godison aliongeza kuwa pamoja na hayo  waajiriwa wote na wanaojiajiri wanatakiwa kuhakikisha wanatanguliza  nidhamu kazini pindi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kazi,sanasana alisema kuwa wale wanaoajiriwa wanatakiwa kuwa makini sana kwenye majukumu yao kwani tofauti na hapo wanaweza  kujikuta  wanaachishwa kazi hususani kipindi hiki cha “hapa kazi tu”.
Pichani: Bwana Godison Rwegasira, Mkurugenzi wa chuo cha King Rumanyika kilichopo Manispaa  ya Bukoba Mkoani Kagera



FAIDA NA CHANGAMOTO ZA KAZI YA BODABODA - KAGERA

Na Frank Johnson
Biashara ya bodaboada ni biashara inayokuwa kwa kasi sana mkoani Kagera,ikianzia nchi ya jirani Uganda na kwa Tanzania naweza sema Kagera ndio Mkoa wa kwanza kufanya biashara hii ya bodaboda.Vijana wengi kutokana na ukosefu wa ajira wameamua kuingia kwenye biashara ya bodaboda.Kwa mkoa wa Kagera biashara ya bodaboda imekuwa ni fursa kwa vijana kutokana na ukosefu wa usafiri wa magari kutoka sehemu moja kwenda nyingine mfano mtu anayetoka Kahororo,Kashai au Mafumbo akitaka kwenda mjini ni lazima achukue bodaboda au atembee kwa mguu.
Gazeti la Hamasa limefanikiwa kuzungumza na waendesha bodaboda pia wamiliki wa bodaboda kujua ni changamoto gani na faida wanazopata kutoka kwenye bodaboda,tulizungumza na waendesha bodaboda kutoka wilaya ya Bukoba,Karagwe,Misenyi,Muleba,Biharamulo,Ngara na Kyerwa.
Kutokana na malezo yao,kwenye kufanya hii biashara ya bodaboda kuna njia mbili,moja ni kumwachia  ni kuwa na mkataba, wamiliki uwapa waendesha bodaboda na uhitaji kupewa kiwango cha pesa kuanzia Tsh 7,000 hadi Tsh 10,000 na baada yamwaka mmoja inakuwa ya muendesha bodaboda baada ya mkataba kuisha,aina ya pili ni bila mkataba mmiliki hupewa kuanzia Tsh 6,000 hadi Tsh 8,000 kwa siku kulingana na eneo husika.
Mkoani Kagera changamoto na faida wanazopata bodaboda tulizobaini kutokana na kufanya nao mahojiano kutoka katika wilaya zote ni,wizi na uporaji umeongezeka,kama ilivyo changamoto kwenye biashara nyingine,waendesha bodaboda wengi wameibiwa na kuporwa pikipiki na watu wanaojifanya kuwa abiria lakini baadaye wanawageuka na kuwapora kwa kuwatishia kuwafanyia jambo baya.
Changamoto nyingine ni ajali kuongezeka,hii inasababishwa na vijana wengi kutokujua sheria za barabara,kuna vijana wanaamini ukishajua kuendesha bodaboda mtaani unaweza pia kuendesha barabarani,hii hupelekea waendeshe pikipiki barabarani bila kuwa na uelewa kuhusu sheria za barabara.Ajali nyingi zimepelekea vifo na ulemavu wa kudumu kuongezeka. Changamoto nyingine waliyotuambia ni kupata vishawishi vya ngono, kuna abiria ambao ni wanawake wakipandapikipiki hawataki kulipa na kuwambia kuwa wanaweza kulipa kwa kufanya ngono hasa abiria ambao wanawachukua usiku kutoka sehemu za starehe.Hii inapelekea magonjwa ya zinaa kuongezeka,mimba zisizotarajiwa na watoto wanaozaliwa kukosa malezi pia ni hasara kwa muendesha bodaboda na mmiliki kwa kukosa mapato sahihi.
Changamoto nyingine tuliyoigundua Hamasa ni kuwa watoto wanaugua ugonjwa wa nimonia kwa kuwekwa mbele kabisa kwenye pikipiki,kutokana na upepo mkali hii inapelekea watoto kupata ugonjwa wa nimonia.
Pia waendesha bodaboda na wamiliki wake mkoani Kagera wametueleza faida wanazopata kutokana na biashara hiyo ya bodaboda. Moja imekuwa mkombozi wa tatizo la ajira,biashara ya bodaboda imeleta ajira kwa vijana,vijana wengi mkoani Kagera wamejiajiri kwenye bodaboda na kuajiriwa pia kutokana na biashara hii,hivyo inawaongezea kipato.Pia imeleta ajira kwa mafundi ambao hutengeneza hizo bodaboda pale zinapoharibika au kuzifanyia matengenezo.
Pili vipato vya ziada vya wafanyakazi binafsi na wale wa serikali kama waalimu vimeongezeka,wafanyakazi wengi wamechukua mikopo na kununua bodaboda ili kuwapa vijana waendeshe kwa ajili ya kuwaongezea kipato cha ziada,wafanyakazi wengi wananufaika kutokana na hii biashara ya bodaboda mkoani Kagera.
Tatu imerahisisha usafiri maeneo ya mjini na vijijini pia,kuna maeneo mengi mkoani Kagera kabla ya biashara ya bodaboda kuingia wananchi walikuwa wanapata shida ya usafiri na kuwalazimu kutembea umbali mrefu kwa mguu,lakini sasa kutokana na uwepo wa bodaboda imerahisha usafiri mjini na vijijini. Mwisho serikali imeingiza mapato na inazidi kuingiza

mapato kutokana na biashara hii ya bodaboda, kuanzia pikipiki zinapoingia Tanzania hadi biashara inapofanyika.
Hasara ya hii biashara ni kwamba imesababisha vilema vingi sana, watu wengi wamepata vilema kutokana na matumizi mabovu ya usafiri huu.
Gazeti la Hamasa linatoa wito kwa serikali ya mkoa wa Kagera kuwa wanatoa elimu mara kwa mara kwa waendesha bodaboda kuhusu usalama barabarani pia wamiliki wa bodaboda kuhakikisha mtu wanayempa chombo cha usafiri ana leseni.Vilevile tunatoa wito kwa waendesha bodaboda kuzingatia sheria za barabarani na kutotumia kilevi chochote muda wa kazi.

Madereva bodaboda wakiwa wamepack jirani na soko kuu la manispaa ya Bukoba