![]() |
Muonekano wake kabla gazeti halijawa printed |
![]() |
Mbunge wa Bukoba Mjini (katikati), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media kwa pamoja wakisaini 'MoU |
'
![]() |
Semina ikiendelea |
![]() |
Washiriki wa semina katika Picha ya pamoja |
Hii ni taarifa rasmi iliyochapishwa kwenye Toleo la Pili la Gazeti la Hamasa
Jamii Media,
waendeshaji wa mtandao maarufu kwa JamiiForums walikuwa mjini Bukoba kwa siku
tatu mfululizo kuanzia Tarehe 3 hadi 5 Agosti, 2016 kwa ziara maalum ya
uzinduzi wa Mradi uitwao Tushirikishane.
Mradi huo ambao upo
katika hatua ya majaribio una malengo ya kuwasaidia viongozi wa kuchaguliwa na
wananchi hususani wabunge kutekeleza ahadi walizotoa wakati wa kampeni za
uchaguzi mkuu uliopita kwa urahisi. Pia mfumo shirikishi unaotumika katika
kuendesha Mradi wa Tushirikishane utasaidia Halmashauri
kuboresha na kutoa huduma za jamii kwa ufanisi zaidi.
Akiongea mbele la
Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media na
Mwanzilishi-Mwenza wa mtandao wa JamiiForums, Ndg. Maxence Melo aliwashukuru
viongozi wa Manispaa ya Bukoba, Madiwani na Mbunge Jimbo la Bukoba Mjini kwa
kuupokea mradi wa Tushirikishane na kuonyesha utayari wa hali
ya juu katika kushiriki utekelezaji wake.
Aliongeza kuwa, Tushirikishane itatekelezwa
katika Majimbo Sita(6) na Jimbo la Bukoba Mjini limekuwa la kwanza kuingia
katika hatua ya utekelezaji.
Naye Mbunge wa Bukoba
Mjini, Mh. Wilfred Lwakatare alizisifu jitihada za Jamii Media katika kuchochea
uwajibikaji hususani kwenye sekta ya umma nchini Tanzania. Aliupongeza ubunifu
na dhima iliyomo ndani ya mradi wa Tushirikishane na
kuyafananisha maudhui yake na nadharia ya “Usimamizi Lazimishi”
Katika warsha hii,
washiriki walikuwa ni kutoka makundi yanayowakilisha wadau wakuu wa mradi;
ambayo ni wananchi/wapigakura, viongozi wa kuchaguliwa na uongozi wa
Halmashauri wamepata kujua malengo, muundo wa mradi, wajibu wa wadau na jinsi
ya kushiriki katika hatua na shughuli mbalimbali za mradi. Pamoja na shughuli
hizo, yako matukio mengine makuu mawili yalitendekeka sambamba na warsha hii
katika kuelekea kwenye utekelezaji wa mradi.
Washiriki walipata
kupitia ahadi zilizotolewa na mgombea aliyeshinda kiti cha Ubunge, jimbo la
Bukoba Mjini na kuchagua ahadi kuu tatu kwa umuhimu zinazoweza kutekelezeka
ndani ya miezi tisa toka sasa.
Ahadi zilizochaguliwa
ni fungu la kwanza linajumuhisha Ujenzi wa Kituo cha Mabasi Kyakailabwa, ujenzi
wa Soko-Kuu la Bukoba na soko la Kashai, namba mbili ni kuwawezesha vijana na
akinamama kujiajiri kwa kuwapa mikopo ya riba nafuu na mwisho ni kurasimisha
makazi na maeneo mapya.
Pamoja na vipaumbele
hivi, Mh. Lwakatare na Madiwani walikubaliana kuwahamasisha wakazi wa Jimbo la
Bukoba Mjini kujiunga na mifuko ya Bima ya Afya. Suala hili limekubalika kuwa
mtambuka na hivyo litakuwa mada ya kudumu katika mikutano ya hadhara na ziara
za viongozi.
Warsha ya Tushirikishane ilienda
mbali zaidi kwa kuandaaa Mpango-Kazi wa utekelezaji wa ahadi zilizochaguliwa
kutekelezwa chini ya usimamizi wa mradi. Ili kuhakikisha pande zote
zinazohusika katika Mradi zinatekeleza makubaliano, randama (Memorandum of
Understanding) ilisainiwa kati ya Ndugu Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Jamii Media ambaye atatambulika kama msimamizi na muendeshaji wa mradi, Mh.
Wilfred Lwakatare Mbunge Jimbo la Bukoba Mjini - mhusika mkuu katika
utekelezaji wa ahadi, na Mstahiki Meya, Chief Karumuna kwa
niaba ya Baraza la Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba ambalo lina jukumu la
kuhakikisha huduma za jamii na Sheria ndogondogo zinaboreshwa.
Jamii Media pia
ilimtangaza Mhadhiri Happiness Essau na kumuwezesha kwa kumpatia vitendea kazi
vitakachomuwezesha kufanya kazi za Afisa Mawasiliano wa Mradi katika Jimbo la
Bukoba Mjini kwa ufanisi. Mhadhiri Happiness atakuwa na jukumu la kukusanya na
kusambaza habari zilizothibitishwa juu ya maendeleo ya utekelezaji wa
Mpango-Kazi.
Njia zitakazotumika
kupashana habari ni pamoja na mitandao ya kiganjani (WhatsApp, Telegram), uzi
maalumu kwenye tovuti ya JamiiForums.com, makala kupitia FikraPevu.com, kurasa
za mitandao ya Twitter, Facebook, Instagram zinazomilikiwa na Jamii Media na
kupitia vyombo vingine vya habari.
Gazeti lako pendwa la
HAMASA ni mdau aliyeidhinishwa kutoa taarifa rasmi juu ya maendeleo ya mradi wa
Tushirikishane kwa Jimbo la Bukoba Mjini. Wananchi na wadau wenye kiu ya kuiona
Bukoba ikipiga hatua kimaendeleo wanakaribishwa kuitumia HAMASA kuonyesha jinsi
gani Tushirikishane inaweza kupanuliwa kwa faida kubwa zaidi.

- MWISHO -
No comments:
Post a Comment