Tuesday, September 20, 2016

MAONI YA MDAU: MAENDELEO HAYALETWI NA MAKONGAMANO

Mkoa wa Kagera ni mojawapo ya mikoa kongwe kabisa hapa Tanzania. Hapo mwanzo ulijulikana kwa jina la Mkoa wa Ziwa Magharibi kumaanisha ni mkoa ulio karibu na Ziwa Victoria. Mkoa huu umejaaliwa kila aina ya neema na rasilimali. Kilimo cha ndizi na kahawa ndiyo mazao makuu kwa ajili ya uchumi wa wanaKagera. Kwa upande mwingine mkoa huu umejaaliwa shughuli za uvuvi unaoendelea katika ziwa victoria ambapo  kuna uvuvi mkubwa samaki aina ya sangara, sato na dagaa. Mbali na rasilimali zote hizi kuna watu mashuhuri ambao wametokea katika mkoa huu ambao wamechangia Maendeleo makubwa katika mikoa mingine. Lakini kumetokea changamoto kubwa ya kimaendeleo kiasi kwamba mkoa huu umetajwa kati ya mikoa maskini zaidi hapa Tanzania. Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Philip Mpango alitoa takwimu hizi wakati akiwasilisha taarifa ya tathimini  ya mwaka 2015/2016 alionesha kuwa mkoa huu una umaskini wa asilimia 39.3 wilaya ya Biharamulo inaongoza kwa umaskini zaidi. Takwimu zinaonesha kuwa wakazi wa mkoa huu wana kipato cha chini kabisa na shughuli za uzalishaji haziwaingizii kipato kama inavyostahili kulinganisha na mikoa mingine. Takwimu ya wizara ya fedha inaonesha kuwa asilimia kubwa ya wakaazi wa mkoa huu mbali na kipato cha kila mtanzania kimepanda kutoka shilingi 770,464 mwaka 2010 hadi  shilingi 1,919,928 kwa mwakabado kipato hiki hakijafikiwa na watanzania wengi wa mkoa huu. Hatuwezi kuzibeza wala kuzidharau takwimu hizi kwani zina maana kubwa kwa maisha ya kila siku ya wanaKagera. Na katika kujadili umaskini ni lazima kuweka mapendekezo ya nini kifanyike ili kukinusuru kizazi cha mkoa huu ambao una historia kubwa kwa Maendeleo ya taifa hili.
Kilimo na ufugaji, huu ni utimgongo wa watanzania wengi lakini katika mkoa huu wakulima wengi hawalimi kwa ajili ya biashara bali hulima kwa ajili ya kula tu (subsistence) ambapo inakuwa ngumu kwao kushindana na uzalishaji wa mikoa mingine. Kilimo cha mkoa huu kimekuwa cha mazoea sana kiasi kwamba wakulima hawajibadilisha fikra zao na namna ya uendeshwaji wa kilimo. Zao la ndizi ambalo limetegemewa kwa karne nyingi limekumbana na ugonjwa wa mnyauko(Banana Xanthomonas wilt) ambapo uzalishaji wa ndizi umepungua kwa kasi sana. Kilimo kinapaswa kubadilishwa kwa wakulima kulima mazao mbadala kama viazi, ufuta,mihogo na mazao ambayo sio ya msimu. Aidha kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kwa wananchi kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji. Mkoa huu umejaaliwa mito na mabwawa pamoja na maziwa kadhaa ambayo yanaweza kuwa chanzo cha maji. Mwambao wa Mto Ngono ni mojawapo ya eneo lenye rutuba kubwa kinacho hitajika ni kuweka utaratibu wa vikundi kwenda kuanzisha kilimo cha mazao ambayoyanaweza kuwa ya chakula na biashara pia. Kilimo cha umwagiliaji kinaweza kutatua tatizo la chakula hapa mkoani. Biashara, sekta ya biashara ni moja wapo ya sekta ambayo ina manufaa makubwa sana mkoa huu una bahati ya kuwa mpakani na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda ambazo zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha mahusiano ya kibiashara kwa wakazi wa mkoa huu. Mipaka inapaswa kutumika kama kitovu cha uchumi wa mkoa huu, kuna bidhaa ambazo hazipatikani katika mataifa jirani ambazo wananchi wakihamasishwa wakasafirisha mpaka huko wanaweza kupata masoko pamoja na mahusioano mema ya kibiashara. Lakini pia biashara ya ndani kwa ndani ni mojawapo ya kitu muhimu kwa wananchi pamoja na uchumi wa mkoa mzima. Biashara zote kubwa na ndogo zinapaswa kuwekewa utaratibu mzuri ambao utawanufaisha wafanyabiashara na wananchi. Pia uwekezaji kwenye bidhaa za chakula nafaka pamoja na biashara ambazo zinaendana na kasi ya karne hii. Wadau wa Maendeleo, mkoa huu una watu mbali mbali ambao wameendelea kiuchumi lakini hawajaweza kujiwekeza katika mkoa huu ili  kuwanufaisha wakaazi wa mkoa huu.Aidha juhudi za wadau hawa kamwe hazitoshi, kumekuwa na makongamano pamoja na vikao vya wadau wa Maendeleo wa mkoa huu ambavyo havijazaa matunda kwani ushirikiano unakuwa ni mdogo au ushirikiano na walengwa unakuwa ni mdogo sana. Kwa upande mwingine Maendeleohayawezi kuletwa na watu waliopo mbali ila ni juhudi za watu waliomo ndani ya mkoa kwani waliopo nje huweza kuja wakiona kuwa waliopo ndani wametia nia na juhudi za kujikwamua kimaendeleo.
Uvuvi, sekta ya uvuvi ni mojawapo ya maeneo ambayo yanaweza kulikuza pato la mkoa huu. Kuna maziwa kama Ikimba,Burigi, Victoria pamoja na mito mikubwa ambayo ipo mkoani kama Kagera na Mto Ngono. Lakini kwa takwimu zilizopo ni kwamba samaki wengi wanaotumiwa Rwanda wanasafirishwa kutoka Mwanza jambo ambalo linapaswa kubaki aibu kwa wafanyabiashara na wavuvi wa mkoa wa Kagera. Sio kwamba samaki hawapo ila tatizo ni mfumo wa uvuvi pamoja na mawazo ya wavuvi. Mfano takwimu zinaonesha kuwa kipato cha uvuvi kimeshuka kutoka tani kilo 150 kwa mtumbwi hadi kilo 15 kwa mtumbwi. Njia za uvuvi zinazotumika bado ni za kiasili na wavuvi wengi wamelenga soko la ndani tu. Kilimo cha uvuvi kinapaswa kuimarishwa sana kwa kuhamasisha uvuvi wa kisasa na kuweka misingi ambayo mazao ya uvuvi yatapata soko la ndani na nje.
Kwa upande mwingine mkoa huu una vivutio kadhaa vya utalii ambavyo vikitangazwa  vyema vitakuwa chachu ya kuwaleta watalii na kuinua biashara za mahoteli pamoja na kuutangaza utamaduni wa mkoa wa Kagera. Utamaduni wa ngoma, mavazi chakula vikitumiwa kisawa sawa ni jambo muhimusana katika kuukuza utalii na mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi. Maendeleo ni mojawapo ya kilio cha watanzania wengi, kuna umuhimu mkubwa wa wakazi wa mkoa huu waliopo ndani na nje kuweka na kutekeleza mipango mikubwa kwa ajili ya kuinua kipato chao. Juhudi za serikali pekee hazitoshi kuinua kipato na kuondoa umaskini. Mikoa mingi ambayo imeendelea haijaendelea kwa sababu ya juhudi za serikali ila ni juhudi za wananchi pekee na serikali inakuwa chanzo cha kuweka utaratibu ili mwananchi wanufaike.
 Pia nguvu kazi ambayo ni vijana inapaswa itumike kisawa sawa kwani inaonekana kuwa vijana wengi siku hizi wanakimbilia mijini na kufanya kazi ambazo zinaingiza kipato kwa muda mfupi. Hii hurudisha nyuma uzalishaji wa mazao na chakula. Vijana kama nguvu kazi inapaswa wawe watu wa kwanza kabisa katika mchakato wa kuleta Maendeleo kwa jamii. Vijana wakiwa katika vikundi au mmoja mmoja wawekewe utaratibu mzuri ambao watatumia fursa zilizopo kwa kila mkoa kwa manufaa ya vizazi vijavyo pamoja na kizazi hiki. Pia Maendeleo hayawezi kuletwa kwa vikao na makongamano bali kuna umuhim mkubwa wa kutekelea miradi na mipango ya Maendeleo kwa ajili ya manufaa ya wanaKagera.

Maoni ya WEKISHA K KARUMNA (Mwanafunzi wa UDSM na Mkazi wa Muleba)

No comments:

Post a Comment